Na MWANDISHI WETU,TABORA
Katika kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, Waziri wa Madini Doto Biteko ameitumia fursa hiyo kuwaasa wachimbaji wote wa Madini Nchini kuhakikisha wanalinda afya zao kwa kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
 

Waziri Biteko ameyasema hayo baada ya kutembelea mgodi wa wachimbaji wadogo wa Nsungwa uliopo wilayani Kaliua Mkoa wa Tabora ambako kumeibuka mfumuko wa Madini ya Dhahabu (Rush).
 

Aidha, Waziri Biteko amewataka wachimbaji hao kuhakikisha wanatunza akiba ya kipato wanachokipata na kutunza familia zao ikiwemo kuwekeza katika sekta nyingine hususan katika Sekta ya Biashara na Kilimo.
 

“Hela unayoipata usiidharau hata kama ni kidogo weka akiba ili ije ikusaidie kesho ukiwa huna nguvu, leo unanguvu unaingia duarani lakini baada ya miaka kadhaa hautaweza, utaitaji watu wa kukusaidia, nguvu ya leo uiweke akiba kwa ajili ya kesho ili ikusaidi kuwa na kesho nzuri usije ukawasumbua watu,” amesema Waziri Biteko.
 

Waziri Biteko amesema Wilaya ya Kaliua inafahamika kwa Kilimo cha Tumbaku ambapo kwa sasa umetokea mlipuko wa Madini ya Dhahabu katika eneo hilo na kusababisha Wilaya hiyo kuingia kwenye orodha ya Wilaya zinazochimba Madini ambapo amewataka Wachimbaji hao kuendelea kuwa watulivu na kufuata Sheria katika uchimbaji wao.
 

Pia, Waziri Biteko amesema haki zipo nyingi kuna Haki ya Ardhi, Haki ya Anga, Haki ya Madini na kadhalika, unaweza ukawa na shamba lakini mmiliki mkuu wa shamba hilo ni wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwenye mamlaka ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama kwenye shamba hilo kuna Madini hairuhusiwi yachimbwe mpaka kuwe na leseni katika eneo hilo.
 

“Yoyote anayepewa leseni ya Madini kazi yake ya kwanza ni kwenda kwa mwenye shamba sababu huwezi kuyachimba Madini mpaka ukubaliane na mwenye shamba na kuna makubaliano ya aina mbili ya kwanza ni kumlipa fidia mwenye shamba ili akupishe na aina ya pili ni mwenye shamba kuingia shea kwenye leseni husika,” amesema Waziri Biteko.
 

Pia, Waziri Biteko amewasisitiza wachimbaji wadogo kuachana na suala la kutorosha madini ambapo amewataka kuchimba kwa kufuata Sheria na kuhakikisha kodi ya Serikali inalipwa.
 

“Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anataka kuona Uchumi wa Madini unamilikiwa na Watanzania wa kawaida pia wachimbaji wote walioko sehemu mbalimbali ikiwemo Kaliua wanabadilisha maisha yao kwa rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu amewabariki,” amesema Waziri Biteko.