Kundi la Oromo ambalo linashirikiana na waasi wa Tigray nchini Ethiopia limesema kuwa mji mkuu Addis Ababa huenda ukakamatwa katika miezi au wiki kadhaa, wakati wapiganaji wakisonga mbele kuelekea kusini mwa nchi. 

Jeshi la Ukombozi wa Watu wa Tigray - TPLF, ambalo limekuwa likipigana na serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kwa mwaka mmoja, limedai kukamata maeneo muhimu katika siku za karibuni, pamoja na mshirika wake Jeshi la Ukombozi wa Waoromo - OLA. 

Msemaji wa OLA Odaa Tarbii amesema kundi lake linakusudia kuiangusha serikali ya Abiy, akiita kuondolewa kwake kuwa ni suala lililomazilika kitambo. Matamshi hayo yamekuja saa kadhaa baada ya Ethiopia kutangaza hali ya hatari kote nchini na kuwaamuru wakaazi kujiandaa kuvilinda vitongoji vyao. 

Abiy amewahimiza wananchi kuunga mkono vita na kuwatuhumu waasi kwa kujaribu kuigeuza Ethiopia kuwa Libya na Syria. 

Uchunguzi wa pamoja wa ofisi ya mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet na Tume ya Haki za Binaadamu ya Ethiopia - EHRC umegundua ushahidi wa ukiukaji mkubwa wa haki unaofanywa na pande zote za mgogoro.