Waasi Ethiopia Wazidi kusonga mbele, Waziri Mkuu Abiy Ahmed Kuongoza Mapambano ya Vita
Wakati muungano wa waasi kutoka Tigraya na Oromo wakiwa kilomita 200 na mji mkuu wa Ethiopia, Waziri Mkuu Abiy Ahmed ametangaza kwamba atakwenda kwenye uwanja wa vita yeye binafsi kuongoza ulinzi wa mji mkuu.
Ilikuwa ni baada ya kikao cha kamati kuu ya chama chake, Prosperity Party, ambapo Waziri Mkuu Abiy Ahmed amefahamisha kwamba kuanzia Jumanne hii, Novemba 23, yeye binafsi "atakwenda kuongoza majeshi " katika uwanja wa vita dhidi ya waasi. "Wale wanaotaka kuwa miongoni mwa watoto wa Ethiopia waliosifiwa na historia, simameni leo kwa ajili ya nchi yenu," amesema.
Baada ya kutangaza hali ya hatari Novemba 2, Abiy Ahmed, mwanajeshi wa zamani, amechagua kutoa hotuba ya kitaifa, inayokumbusha viapo vya kulitumikia taifa wakati wa vita vya wafalme wa zamani wa Ethiopia. Kauli hii inakuja, wakati muungano wa waasi kutoka Oromo na Tigray walioapa kumuondoa wamesema wanasonga mbele kuelekea Addis Ababa na hasa tayari wameudhibiti mji wa Shewa Robit, kilomita 200 kutoka mji mkuu.