Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Waajiri wanaoshindwa kuwasilisha vielelezo vya rufaa za Watumishi wa Umma katika Tume ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya kuwezesha maamuzi ya mashauri ya kinidhamu yaliyowasilishwa katika Tume hiyo, wametakiwa kutoa maelezo ya sababu za kutowasilisha kwa wakati vielelezo hivyo.

Akizungumza na Mwenyekiti, Makamishna na Watendaji wa Tume ya Utumishi wa Umma leo jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, haiwezekana Mwajiri amsimamishe kazi Mtumishi wa Umma na kuchukua hatua za kinidhamu halafu ashindwe kuwasilisha vielelezo Tume ya Utumishi wa Umma ili haki itendeke.

“Zipo rufaa nyingi zimewasilishwa Tume ya Utumishi wa Umma bila vielelezo lakini Tume imekuwa ikilalamikiwa kwa kutoshughulikia kwa wakati rufaa hizo, huku kosa likiwa ni la mwajiri kwa kutowasilisha vielelezo kwa wakati, hivyo Serikali haitovumilia jambo hili,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.

Katika kuhakikisha haki inatendeka kwa Watumishi waliochukuliwa hatua za kinidhamu, Mhe. Mchengerwa amemuelekeza Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama kuwasilisha orodha ya Waajiri walioshindwa kuwasilisha vielelezo ili Ofisi yake iwaandikie barua ya kuwataka kutoa maelezo ya sababu ya kutowasilisha vielelezo vya rufaa za Watumishi.

Aidha, Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, Ofisi yake itaandaa Waraka utakaosisitiza Waajiri kuwasilisha vielelezo vya rufaa kwa wakati na pindi watakaposhindwa, zitaandaliwa kanuni za kuiwezesha Tume kuendelea kufanya maamuzi kwa kutumia vielelezo vya upande mmoja ili kuharakisha utoaji wa maamuzi kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.

“Inawezekana rufaa mlizozifanyia kazi leo ni za hivi karibuni, lakini yapo mashauri mengi yaliyowasilishwa muda mrefu na mmeshindwa kuyafanyia kazi kwasababu waajiri hawajawasilisha vielelezo,” Mhe. Mchengerwa ameongeza.

Mhe. Mchengerwa amesema, lazima Serikali isimamie haki za watumishi kwani ndio msingi ambao Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mara kwa mara.

Amesema Serikali haitosita kuwachukulia hatua za kinidhamu Waajiri wote watakaoshindwa kuwasilisha vielelezo vya rufaa za Watumishi wa Umma Tume ya Utumishi wa Umma ambayo ndiyo mamlaka ya nidhamu kwa Watumishi wa Umma.

Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Mchengerwa kuzungumza nao, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Mhe. Steven Bwana amemhakikishia Mhe. Waziri kuwa Tume itaendelea kutoa uamuzi wa haki na kutoa elimu kwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu na Watumishi wa Umma kuhusu uzingatiaji wa Kanuni, Sheria na Taratibu za Kitumishi ili kuhakikisha haki inatendeka.

Ameongeza kuwa, iwapo Tume na wadau wake watatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Kanuni, Sheria na Taratibu za Kitumishi, Serikali itaweza kujenga utumishi wa umma uliotukuka, wenye tija na unaotoa huduma bora kwa wananchi.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Kamishna Khadija Mohammed amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa kuwatembelea na kushuhudia jinsi wanavyofanya kazi, kitendo kinachoonyesha ni kwa kiasi gani anaheshimu majukumu ya Tume ambayo yamejikita katika utoaji haki kwa Watumishi wa Umma.

Kamishna Khadija ameishukuru Serikali kwa kuwaamini na kuwateua kuitumikia Tume kwa kipindi cha miaka mitatu ambacho wameweza kupitia rufaa na malalamiko mbalimbali ya kiutumishi yaliyowasilishwa katika Tume hiyo na kuyatatua kwa njia ya haki.

Mhe. Mchengerwa ameitembelea Tume ya Utumishi wa Umma ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kuhakikisha taasisi zilizo chini ya Ofisi yake zinatekeleza wajibu wake kikamilifu.