Na Selemani Msuya
VIJANA nchini wamesema iwapo Serikali itahakikisha changamoto ya elimu, afya, ajira, uongozi na taarifa zitapatiwa ufumbuzi kundi hilo litaweza kupata maendeleo na kudumisha amani.

Changamoto hizo zimeanishwa na Mwenyekiti wa Ajenda ya Vijana 2020 hadi 2025, Rogers Fungo wakati akizungumza na vijana wenzake jana jijini Dar es Salaam, katika Mdahalo wa Wadau wa Amani uliondaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) na Taasisi ya Kimataifa la Republican (IRI).

Fungo amesema kinachosisitizwa na MNF na IRI ni muhimu kwa uendelevu wa taifa, ila kinaweza kisitoe matokeo chanya kama changamoto za elimu, afya, ajira, uongozi na taarifa hazitapatiwa ufumbuzi sahihi.

“Hoja ya kwamba tushiriki pamoja kudumisha na kuimarisha udugu, uzalendo, uwajibikaji, amani, maridhiano na maendeleo nchini kama mdahalo unavyosema inaweza kuwa na mashiko kama kundi la vijana litatatuliwa changamoto hizo tano nilizozitaja,” amesema.

Akifafanua kuhusu elimu, Fungo amesema inayotolewa nchini haimpi nafasi kijana kuwa mbunifu na muona fursa hivyo kushauri Serikali kuangalia mfumo wa elimu wa sasa.

Aidha, amesema katika eneo hilo kuna changamoto ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu jambo ambalo linaondoa dhana nzima ya kumkomboa kijana kielimu.

Kuhusu changamoto ya afya alitoa rai kwa Serikali kuangalia uwezekano wakuwapatia vijana wote bima ya afya ili wawe sehemu sahihi ya kujenga amani, umoja, uchumi na maendeleo ya nchi.

“Katika eneo la ajira hapa kuna changamoto kubwa kwani pamoja na vikwazo vilivyopo kwenye elimu na afya, kuna kundi kubwa linazalishwa na vyuo vyetu ambapo takribani vijana 800,000 wanaingia kwenye ajira kila mwaka ila wanaojiriwa hawazidi 40,000 hivyo kuna vijana zaidi ya 760,000 wanazagaa mitaani ni tatizo kubwa,” amesema.

Mwenyekiti huyo amesema Serikali inapaswa kuagiza taasisi na ofisi mbalimbali kutumia ofisi za umma kuhamasisha vijana kuomba mikopo ili waweze kujiajiri.

Aidha, kuhusu kadhia ya uongozi amesema bado ushirikishwaji wao umekuwa duni katika nafasi hivyo juhudi ziongezeke ili waweze kuchangia kudumisha umoja, amani na maendeleo kama MNF inavyosisitiza.

Fungo amesema yote ambayo ameyaanisha yanaweza kuwa na faida iwapo taarifa sahihi kwa wakati sahihi zitatolewa na mamlaka husika ili vijana waweze kutumia fursa zilizopo.

Naye Katibu wa Kamati ya Amani Tanzania, Joseph Malekela amesema Tanzania itaendelea kuwa na amani, umoja na maendeleo iwapo dhana ya udugu, uzalendo, uwajibikaji itapata nafasi katika hatua yoyote ambayo vijana wanachukua.

Malekela amesema vijana pamoja na kuwa na changamoto zao binafsi lakini wameshindwa kuishi kwa udugu na umoja ambapo sababu kubwa ni ubinafsi na utandawazi kuchukua nafasi zaidi.

Akichangia katika mdahalo huo wa wadau wa amani Mrajisi wa Jumuiya Zisizo za Kiserikali Zanzibar, Ahmed Abdul amesema jukumu la kuitunza amani ya Tanzania lipo kwa Watanzania wote ila vijana ni nguzo muhimu zaidi.

Mrajisi huyo amesema iwapo vijana wa Kitanzania watshiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa amani na umoja wa nchi maendeleo yatapatikana kwa haraka.

“Kwetu Zanzibar tumezingatia misingi ya umoja na amani ndio maana leo unaona tuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ila hili limefanikiwa kwa sababu vijana wamekuwa sehemu ya makubaliano hayo hivyo naomba vijana tusimamie misingi hiyo,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MNF, Joseph Butiku amesema taasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake imejikita katika kujenga umoja, amani na maendeleo kwa nchi na wananchi hivyo ni imani yao kupitia vijana ujumbe utafika kila mahali.

Amesema Hayati Mwalimu Nyerere wakati akianzisha taasisi hiyo alitamani kufanikisha yale ambayo alishindwa kuyafanikisha wakati wa uongozi wake kama Rais hivyo nao watahakikisha wanasimamia misngi hiyo kwa maslahi ya nchi.

Butiku amesema wameandaa midahalo iliyoshirikisha makundi ya kisiasa, dini, asasi za kiraia na vijana lengo likiwa ni kutoa fursa kwa kila mdau kushiriki kujenga amani ya nchi.