Uwekezaji kwenye zao la dagaa ni muhimu kiafya kwa kuwa utasaidia wananchi kuondokana na utapiamlo lakini pia utawanyanyua wananchi kiuchumi.

Hayo yamesemwa   na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega wakati alipotembelea mialo ya Igabilo na Rushara iliyopo wilayani Bukoba mkoa wa Kagera kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wavuvi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi, Ndugu Shaka Hamdu Shaka.

Naibu Waziri Ulega amesema dagaa watasaidia sana kuondoa utapiamlo kwa kuwa wana protini, madini ya chuma na madini mengine ambayo ni muhimu kwa afya ya binadamu. Pia amesema itawashangaza sana watu endapo maeneo ambayo kuna dagaa wengi watoto wawe na tatizo la utapiamlo. Hivyo wavuvi wamehimizwa kutumia njia bora za uanikaji wa dagaa ikiwa ni pamoja na kuwahifadhi vizuri ili wasipoteze ubora.

Vilevile wavuvi na wafanyabiashara wa dagaa wamehimizwa kuwekeza katika zao hilo ili waweze kuvua kwa wingi, waweze kuwahifadhi kwa kuzingatia ubora na kuwasafirisha katika maeneo yote ya nchi ili wananchi wengi waweze kununua dagaa kitu ambacho kitawaongezea kipato hasa ikizingatiwa kuwa watu wengi wanahusika katika mnyororo mzima wa thamani wa dagaa.

Akiwa katika mialo hiyo, Naibu Waziri Ulega aliwasihi wavuvi kujiunga kwenye ushirika ili waweze kuunganishwa na taasisi za fedha ambapo itakuwa ni rahisi kwa wao kupata mikopo ambayo itawasaidia kuweza kununua zana bora za uvuvi na kuanza kuvua kisasa.