Mkutano Mkuu wa 41 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), umepitisha tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa twitter wa ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa, azimio   la kuitangaza siku hiyo limepitishwa na wanachama wote bila kupingwa siku ya Jumanne Novemba 23, 2021 katika kikao kilichofanyika Paris, Ufaransa.

Hatua hii inakifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza Afrika kutambulika na Umoja wa Mataifa na chenye siku maalumu ya kuadhimishwa.

Kiswahili hadi sasa tayari kinatambulika kama miongoni mwa lugha rasmi kwenye Muungano wa Afrika, na kinatumika kama lugha rasmi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na bunge la Afrika na ni moja ya lugha za Afrika zinazozungumzwa na watu wengi duniani.

Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa umetoa taarifa na kusema: "Hizi ni miongoni mwa jitihada za serikali ya Tanzania katika kukikuza Kiswahili na kuenzi urithi tulioachiwa na muasisi wa taifa letu Mwalimu J.K Nyerere."