Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amepiga marufuku uanzishwaji holela wa masoko na minada ya  mazao ya mifugo na uvuvi ambapo amesema masoko na minada hiyo inatumiwa na wafanyabiashara  kukwepa kulipa kodi ya Serikali.

Ndaki ameyasema hayo jana (06.11.2021) wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya makusanyo ya maduhuli ya sekta ya Uvuvi kutoka kwa Maafisa wafawidhi wa vituo vya ulinzi wa rasilimali za uvuvi  nchini kilichofanyika kwenye hoteli ya Morena jijini Dodoma.

“Kiutaratibu ni lazima tukague na tusajili masoko na minada yote hapa nchini lakini Kuna watu wanajianzishia tu masoko kule halafu analiita soko lake la kimataifa, hapana hatuwezi kuendelea na hiyo habari ni lazima sheria na taratibu zifuatwe” Ameongeza Ndaki.

Ndaki amemuelekeza katibu Mkuu wa wizara hiyo anayesimamia sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah kupitia upya masoko yote ya mazao ya uvuvi yaliyopo hapa nchini na kujiridhisha kama yanastahili kusajiliwa nay ale ambayo hayastahili yafutwe mara moja.

“Kinachosikitisha ni kwamba, huko wanakoanzisha haya masoko na minada hakuna wataalam wetu hivyo kila mtu anaenda sokoni na kuchukua anachotaka bila kufuata utaratibu wowote ule, hatuwezi kuwa na serikali ya namna hiyo na Mhe. Rais hatotuelewa ikiwa kila mahala tutakuwa na masoko na minada inayoendesha shughuli zake kiholela” Amesisitiza Ndaki.

Wakati huo huo Ndaki amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo  anayesimamia sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah kuwaandikia barua ya onyo maafisa wafawidhi wa vituo vyote vilivyokusanya maduhuli chini ya asilimia 50 ya lengo walilowekewa ambapo amesema kuwa hatua zaidi dhidi ya maafisa hao zitachukuliwa endapo hawatoongeza kiwango hicho.

“Ila huyu wa Mtera ambaye ameshindwa kukusanya hata shilingi, Katibu Mkuu naomba umuondoe kule na umpangie kazi nyingine kwa sababu ameshaonesha wazi kuwa kazi hiyo imemshinda” Amesema Ndaki.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesisitiza kupitiwa upya kwa kanuni zinazoongoza biashara ya mazao ya uvuvi nchini ambapo amesema kuwa zilizopo haziendani na mahitaji ya soko kwa hivi sasa.

“Samaki wengi hawaingii viwandani kwa sababu ya mabadiliko ya kanuni tuliyoyafanya mwaka 2020 hivyo ninashauri tuboreshe kanuni hizo kwa sababu tumeshaona hasara kubwa tunayoipata na kama hivi viwanda vikifungwa kwetu itakuwa ni aibu na fedheha,   kuna viwanda visivyo vingi visivyo rasmi katika ukanda wa ziwa Victoria kwa ambavyo vinahifadhi samaki aina ya sangara kwenye ubaridi bila kumchakata na ukichunguza utaona hawalipi hata ushuru wa Serikali  ” Amesisitiza  Ulega.

Ulega amemuomba Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki kuridhia mapitio ya kanuni hizo ili ziweze kufanyiwa mabadiliko huku akitolea mfano wa kanuni ya “whole fish” ambayo amesema kuwa inapaswa kufanyiwa mabadiliko na kusimamiwa ipasavyo ili samaki aina ya sangara aweze kuchakatwa na hatimaye Serikali kunufaika na  tozo 13 zinazotokana na uchakataji huo.

“kwenye hii biashara ya mabondo Mhe. Waziri mbali na kupoteza hizo tozo 13 pia tunapoteza nafasi za ajira kwa watu ambao wangehusika na uchakataji wa samaki hawa hivyo ni lazima turudi na kupitia upya kanuni zetu ili tuweze kwenda sambamba na uchumi wa blue” Amemalizia Ulega.

Akielezea sababu za kutofikisha lengo la makusanyo, Afisa Mfawidhi wa kituo cha Ulinzi wa rasilimali za Uvuvi kilichopo mpaka wa Tunduma, Francis Mpatama amesema kuwa hali hiyo imetokana na kitendo cha ofisi yake kuhamia mpakani badala ya ndani kidogo ya nchi ya Malawi alipokuwa akikusanyia hapo awali ambako ndiko kwenye wanunuzi wengi wa dagaa wanaotoka Tanzania.

Naye Afisa Mfawidhi kutoka kituo cha Namanga, Christine Maganga amesema kuwa kushuka kwa makusanyo ya maduhuli katika kituo chake kulitokana na kitendo cha kufungwa kwa ziwa Eyasi ili kuongeza wingi wa samaki katika ziwa hilo.

“Sababu nyingine Mhe. Waziri ni mlipuko wa ugonjwa wa Uviko 19 ambapo idadi ya wateja ilipungua hasa wale wanaotoka nje ya nchi kutokana na taratibu zilizokuwa zimewekwa nchini mwao” Amesema Maganga.

Kikao cha kupokea taarifa ya makusanyo ya maduhuli hufanyika kila robo ya mwaka kwa lengo la kutahmini hali ya makusanyo kulingana na malengo ambayo yamewekwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.