Hafsa Omar-Dar es Saalam

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema Tanzania itaendelea kuendeleza vyanzo vya umeme wa Upepo na umeme wa Jua (solar) ili kuwa na vyanzo vingi vya uzalishaji wa umeme nchini.

Ameyasema hayo, Novemba 18, 2021 wakati akiwa na kikao na balozi wa Denmark nchini Tanzania,  kilichofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati, jijini Dar es Saalam.

Akizungumza katika kikao hicho alisema, kutokana na ongezeko la mahitaji wa umeme nchini lazima kuwepo na vyanzo vingi vya uzalishaji wa umeme ambavyo vitasaidia na vitaweza kutosheleza upatikanaji wa umeme nchini.

Aidha, amewataka wawekezaji wenye uwezo kuwekeza kwenye sekta ya Nishati jadidifu katika maeneo mbalimbali nchini ili kuweza kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.

Pia, ameutaka ubalozi huo, kushirikiana na Tanzania katika kuwajengea uwezo waatalamu wa hapa nchini katika masuala ya teknolojia ya Nishati jadidifu.

Vilevile, amewataka wawekezaji mbalimbali kuanzisha viwanda vya kutengeneza vifaa ambavyo vitavyotumika kwenye uzalishaji wa Nishati jadidifu, vifaa hivyo ambavyo vitawasaidia watumiaji mbalimbali katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Balozi wa Denmark nchini, Mette Norgaard Dissing Spandet, alisema nchi yake kama mdau mkubwa wa maendeleo wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza sekta ya Nishati hasa kwa upande wa Nishati jadidifu.

Alisema, kuwa wawekezaji kutoka Denmark wapo tayari kuja kuwekeza nchini katika sekta ya Nishati hususani kwa upande wa kuzalisha umeme kwa kutumia Upepo.