Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 9/10/2021 nilisitisha kwa muda matumizi ya mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Ukusanyaji Ushuru wa Maegesho ya Vyombo vya Usafiri unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) yaani TARURA e – Revenue Management Information System (TeRMIS) ikiwa ni baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu mfumo huo.

Sambamba na hilo, nilimwelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI kukutana na wataalamu wa TARURA ili kuzifanyia kazi changamoto zilizobainishwa na baadhi ya wananchi kuhusiana na mfumo huu.
 

Ndugu Wanahabari
Kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura 290, Ushuru wa Maegesho ni chanzo cha Mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Ikumbukwe kuwa Ushuru huu umekuwa ukitozwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mujibu wa Sheria Ndogo zilizokuwa zinatungwa na Mamlaka husika. Hata hivyo kuanzia mwaka 2017 baada ya Serikali kuanzisha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), mamlaka ya kusimamia ushuru huo yalihamishiwa kwa TARURA kwa mujibu wa Amri ya Uanzishwaji wa TARURA kupitia Tangazo la Serikali Namba 211 la tarehe 12/5/2017 ambapo kwa kifungu cha 8.1 (vi) cha amri hiyo imebainisha kuwa ushuru wa maegesho ni moja ya chanzo cha mapato ya TARURA. Na kazi hii imekuwa ikifanyika kwa kutumia ukusanyaji wa fedha taslimu (Manual).
 

Utararibu huo ulisababisha changamoto mbalimbali ikiwemo upotevu wa mapato ya serikali, matumizi ya fedha mbichi kabla ya kupelekwa benki, baadhi ya wananchi wasio waaminifu kukwepa kulipa ushuru wa maegesho na pia kusababisha usumbufu na kero kwa wananchi wakati wa ukusanyaji wa ushuru huu ikiwemo magari kufungwa minyororokutokana na ukiukwaji mbalimbali wa taratibu za maegesho zilizowekwa.
 

Ndugu Wanahabari,
Katika kukabiliana na changamoto hizi, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ulitengeneza mfumo wa kielektoniki ujulikanao kama TARURA eREVENUE MANAGEMENT INFORMATION SYSTEM (TeRMIS) kwa ajili ya usimamizi wa shughuli za mapato zilizo chini ya TARURA ikiwemo utozaji wa tozo za maegesho (Parking Fees) ya magari na matumizi ya hifadhi za barabara. Dhumuni la uundaji wa mfumo wa TeRMIS ni kuimarisha ufanisi katika usimamizi wa shughuli za mapato ya Serikali zilizo chini ya TARURA pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwepo kabla ya mfumo wa TeRMIS ikiwemo usimamizi wa tozo za maegesho ya vyombo vya moto na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za Serikali kwa kuhakikisha malipo yote yanafanyika moja kwa moja katika akaunti za Serikali bila kupita kwa wakala au mkusanyaji wa ushuru.
 

Ndugu wanahabari, mfumo wa TeRMIS umeshasimikwa na ulianza kutumika katika Mikoa mitano ya Iringa, Singida, Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam. Hata hivyo katika utekelezaji wa Mfumo wa TeRMIS tumepokea malalamiko ya uwepo wa kero kuhusu mfumo huo hususani kwa Mkoa wa Dar es salaam. Hivyo, ilinilazimu kuchukua hatua ya kusitisha kwa muda matumizi ya mfumo huo tarehe 9/10/2021.
 

Ndugu Wanahabari
Nilimwelekeza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI ashirikiane na TARURA kutatua changamoto kazi changamoto zilizojitokeza katika matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji ushuru wa maegesho na ufuatao ni utekelezaji wa maelekezo yangu.
 

I. Wateja kutopatiwa taarifa za kudaiwa ushuru wa maegesho kwa wakati:
 

Utatuzi
Changamoto hii imetatuliwa na wateja watapatiwa ankara itakayoonesha muda, kiasi anachodaiwa, tarehe na eneo pindi watakapo tumia maegesho.
 

II. Kiwango kikubwa cha gharama za maegesho:
Utatuzi

Changamoto hii imefanyiwa kazi na Kanuni zinazosimamia maegesho zimeboreshwa ambapo kwa Mkoa wa Dar es salaam mtumiaji wa maegesho atatakiwa kulipia shilingi 500 kwa saa na shilingi 2,500 kwa siku tofauti na zamani ambapo mteja alilipia shilingi 500 kwa saa na shilingi 4500 kwa siku.
 

Kwa jiji la Mwanza na Arusha malipo yatakuwa shilingi 500 kwa saa na shilingi 1,500 kwa siku ambapo kwa Manispaa zote na Majiji yaliyobaki malipo yatakuwa shilingi 300 kwa saa na shilingi 1000 kwa siku. Halmashauri za Miji malipo yatakuwa shilingi 500 kwa siku.
 

Viwango hivi vimezingatia vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uhitaji mkubwa wa maeneo ya maegesho ya magari katika mji husika. Aidha viwango hivi vimezingatia kutoa fursa kwa wananchi kuwa na uhuru wa kuegesha na kulipia kwa saa au kwa siku.
 

III. Muda wa kulipa: hapo awali mtumiaji wa maegesho alitakiwa kulipa ushuru ndani ya siku 7 tangu alipotumia maegesho na endapo atashindwa kulipa ndani ya muda huo alipaswa kulipa mara mbili ya ushuru aliokuwa anadaiwa. Na endapo atazidisha siku 14 pia alitakiwa Ushuru wa Maegesho pamoja na faini ya shilingi 30,000.

Utatuzi

Mtumiaji wa maegesho sasa atatakiwa kulipa ushuru ndani ya siku 14 badala ya siku 7 tangu alipotumia maegesho na endapo atashindwa kulipa ndani ya muda huo atatakiwa kulipa Ushuru wa Maegesho pamoja na faini ya shilingi 10,000 badala ya shilingi 30,000 zilizokuwa zikitozwa hapo awali. Hivyo adhabu wa shilingi 30,000/- nimeifuta.
 

Aidha, adhabu ya kuongezeka kwa deni baada ya siku saba iliyokuwepo awali nimeifuta.
 

Vilevile, nimemwelekeza Katibu Mkuu OR – TAMISEMI na Mtendaji Mkuu TARURA washirikiane na Wataalamu wa ofisi zao kuhakiki madeni yote yaliyozalishwa wakati wa utekelezaji wa mfumo wa TeRMIS na kuwasilisha kwenye Mamlaka husika maombi ya kufuta madeni yenye changamoto zilizotokana na matumizi ya mfumo kuanzia siku ambayo mfumo ulianza kutumika.
 

IV. Baadhi ya Wateja kushindwa kulipa kwa kukosa kumbukumbu namba (Control number) na Kumbukumbu namba kutotambuliwa pale wanapotaka kulipa:
Utatuzi:
Ofisi ya Rais ya Rais TAMISEMI, TARURA kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango wameboresha mfumo, sasa kumbukumbu namba (Control number) itapatikana ndani ya dakika moja kwa kutumia njia zifuatazo;
 

a. Kutolewa Ankara kupitia kwa Mkusanya Ushuru
b. Kwa kutumia TeRMIS App. (Inayopatikana PlayStore)
c. Kwa kutumia GePG Tanzania (Inayopatikana PlayStore & AppStore)
d. Kwa kutumi simu ya kawaida Bonyeza *152*00# fuata maelekezo
e. Kwa kutumia Wavuti ya mfumo inayopatikana kwa https://bit.ly/3wjEQSg

Aidha tatizo la kumbukumbu namba kutotambulika pale mteja anapohitaji kulipia limetatuliwa katika mfumo.
 

V. Lugha mbaya kwa wateja kutoka kwa baadhi ya wakusanyaji wa ushuru ya maegesho na kuchukua fedha taslim kutoka kwa wateja:
Utatuzi:
Nimemulekeza Mtendaji Mkuu wa TARURA kuchukua hatua za haraka kwa mawakala watakaothibitika kuwa na wafanyakazi wenye tabia na vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kusitisha mikataba yao mara moja.
 

VI. Utoaji wa elimu kwa umma:
Utatuzi:
Nimewaelekeza TARURA kuandaa mpango kazi utakaohakikisha njia zote muhimu za utoaji wa elimu zinatumika ili kumfikia kila mwanachi kuhusu suala hili. Na Utekelezaji wake uanze mara moja na sio chini ya siku 21 kabla ya kuanza kutumika tena kwa mfumo wa Termis.
VII. Huduma kwa mteja:
 

TARURA wameboresha eneo hili kwa kuanzisha Dawati la Malalamiko na kuweka namba za simu ambazo ni 0733-149658, 0733–149659 au 0733149660 na kupitia namba hizi mteja atapiga simu na kutatuliwa changamoto yake.
 

Pia anaweza kuwasilisha lalamiko lake katika Ofisi za TARURA zilizopo karibu yake (katika Mikoa na Halmashauri).

Ndugu Wanahabari,
Ukusanyaji wa Ushuru wa Maegesho ya magari kwa kutumia mfumo wa TerMIS utapunguza mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali na kuwezesha fedha hizo kuingia moja kwa moja Serikalini. Kutokana na umuhimu wake na kwa kuzingatia kuwa changamoto zilizojitokeza zimeshafanyiwa kazi. Ninarejesha matumizi ya Mfumo huu kuanzia tarehe 1 Desemba 2021. Nitumie fursa hii kuwasihi wananchi hususani wanaotumia magari kutoa ushirikiano wa kutosha mara tu mfumo huu utakapoanza kutumika hapo tarehe 1 Desemba, 2021.
 

Aidha, ninawataka TARURA kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi hasa kwa Mikoa ilioanza kutumia mfumo huu ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam, Mwanza, Singida, Iringa na Dodoma ili kuwepo na uelewa wa kutosha kabla ya kuanza tena kwa matumizi ya mfumo huu.
 

Ndugu wananchi, katika kufikia azma ya Rais Samia Suluhu Hasssan ya kuhakikisha usafi na usalama wa miji, Ofisi ya Rais TAMISEMI inakamilisha taratibu za kuhakikisha kuanzia mwaka wa fedha 2022/23 sehemu ya mapato yatokanayo na ushuru wa maegesho ya magari (angalau asilimia 40) yanagawiwa kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa unapokusanywa ushuru huo. Na fedha hizi zitatumika kwa ajili ya kugharamia usafi wa barabara, Mifereji na uwekaji na uendeshaji wa taa za barabarani katika Mamlaka husika.
 

Hatua hii itaiwezesha TARURA kujikita katika jukumu lake la msingi la ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja ya Mijini na Vijijini.
 

Mwisho;
Kwa kuwa changamoto zilizojitokeza zimeshafanyiwa kazi, nimeridhia kuwa mfumo wa ukusanyaji Ushuru wa Maegesho kwa njia ya kielektroniki (TeRMIS) uanze kutumika tena kuanzia tarehe 1 Desemba, 2021 katika maeneo yote ambapo mfumo huu umefika.
 

Aidha, kwa kuzingatia tija iliyobainika ya mfumo huu nawaelekeza Katibu Mkuu OR – TAMISEMI na Mtendaji Mkuu TARURA waone uwezekano wa kutumia mfumo wa TeRMIS kukusanya ushuru wa maegezo katika Mikoa mingine
 

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

Ummy A. Mwalimu (Mb)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS - TAMISEMI
05 Novemba, 2021