Shirika la afya duniani WHO limetahadharisha kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Covid-19 barani Ulaya huenda ikapindukia watu milioni 2.2 katika msimu huu wa baridi kali iwapo hali ya maambukizi itaendelea kuongezeka. 

WHO imesema watu 700,000 zaidi katika nchi za Ulaya huenda wakafariki kutokana na virusi vya Corona ifikapo Machi 1, 2022 kando na watu milioni 1.5 ambao tayari wamekufa baada ya kuambukizwa virusi vya Corona. 

Shirika hilo la afya duniani pia linatarajia ongezeko la wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura katika nchi 49 kati ya 53 za Ulaya kati ya sasa na mwezi Machi mwaka ujao. 

Mataifa kadhaa ya Ulaya yameshuhudia ongezeko la wagonjwa wa Covid-19, wakati Austria ikiweka vizuizi vipya vya kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo unaoshambulia mapafu. 

Ujerumani na Uholanzi zinajitayarisha kutangaza vizuizi vipya vya kukabiliana na virusi vya Corona.