Shirika la Afya Duniani WHO limetahadharisha juu ya uhaba wa sindano za chanjo na kutishia kukwamisha juhudi za utoaji wa chanjo dhidi ya Covid-19. 

Mtaalamu wa shirika hilo Lisa Hedman amesema Jumanne mjini Geneva kuwa huenda kukatokea upungufu wa sindano kati ya bilioni 1 hadi 2 mwaka ujao. Bi. Hedman ameonya kuwa nchi maskini ndio huenda zikakabiliwa na uhaba mkubwa wa sindano. 

WHO imetoa wito kwa mataifa duniani kuchukua tahadhari mapema kwa kuagiza sindano kwa wingi kutoka makampuni yanayotengeneza sindano. Shirika hilo la afya duniani linakadiria kuwa takriban sindano bilioni 16 zinatumika kwa mwaka. 

Kabla ya janga la ugonjwa wa Covid-19, WHO imesema zilitumika takriban sindano bilioni 1.6 lakini tangu kuzuka kwa janga hilo la kilimwengu, sindano bilioni 6.8 zilitumika kwa ajili ya kutoa chanjo dhidi ya maradhi hayo yanayoshambulia mapafu.