Serikali wilaya ya Bukoba imetakiwa kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua wataalam waliohusika kuisababishia hasara serikali ya milioni 590 kwa kutekeleza mradi wa maji wa Katale chini ya kampuni ya ujenzi ya STC ambao hautoi maji miaka miwili tangu kukamilika kwake na kukabidhiwa.  

Maelekezo hayo yametolewa na katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka alipokuwa kwenye ziara ya uimarishaji wa chama na ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2020-2025.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuitekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM kwa kuhakikisha kaya nyingi zaidi zinafikiwa na huduma ya maji safi na salama sasa ili kuunga mkono dhamira hiyo lazima wataalam wanaohusika na utafiti wa vyanzo vya maji, wanaofanya makadirio ya ujenzi na wakandarasi ujenzi wa miradi hiyo kuwa waadilifu, wazalendo na weledi ili kuiepusha serikali na hasara kwa kuwekeza fedha nyingi kukamilisha miradi bila matokeo ya huduma kwa wananchi.

"Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 ibara ya 100 imetoa maelekezo kwa Serikali ya kuwafikishia wananchi wengi zaidi huduma ya maji safi na salama kwa kuongeza utafiti wa kubaini vyanzo stahiki vya maji, kufanya madirio ya ujenzi pamoja na kuikamilisha miradi ili kutoa huduma. Sasa, ili tufanikiwe lazima wataalam wetu na wakandarasi wanaopewa kazi hizi wawe wazalendo, waadilifu na wenye weledi kuiepusha serikali na hasara" alisema Shaka.

Amefahamisha kuwa Miradi ya aina hiyo inayotumia fedha nyingi bila kutoa huduma inashusha heshima ya chama na serikali jambo ambalo sio CCM wala Rais Samia yupo tayari kuona likitokea hivyo amelekeza  hatua stahiki zichukuliwe kwa wote wataobainika kuhujumu  mradi huo.

"Kukosekana kwa maji safi na salama ni kuongeza umaskini wananchi wanatumia muda mrefu kutafuta maji kuliko kushiriki shughuli zao za kiuchumi pamoja na kutumia fedha nyingi kujitibu maradhi yatokanayo na matumizi ya maji ambayo sio salama" alisema Shaka

Shaka ameahidi kuwa CCM itatoa msukumo kwa wizara ya maji kuleta shilingi milioni 50 kwa ajili ya kurejesha huduma ya maji Katale na nitoe  rai kwa mameneja wa Ruwasa Mikoa na wilaya kuongeza umakini katika ufuatiliaji na usimamizi wa miradi ya maji ili kuleta ufanisi na tija kwa wananchi.

Kaimu Meneja wa Ruwasa halmashauri ya wilaya ya Bukoba Ndugu Evaristo Mgaya alimueleza Ndugu Shaka kuwa miongoni mwa changamoto zinazoukabili mradi huo ni wananchi wa eneo hilo kuharibu miundombinu ya maji pamoja na uhitaji wa fedha milioni 50 ili kurejesha huduma.

Hata hivyo Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza alisema ni miaka miwili sasa wananchi wa Katale wanatembea umbali mrefu kufuata maji ambayo sio salama achilia mbali serikali kukamilisha mradi huo wa milioni 590 bila kutoa huduma kwa wananchi hivyo kuomba chama cha Mapinduzi kiingilie kati suala hilo ili kuwanusuru na kadhia hiyo wananchi anaowawakilisha bungeni.

Shaka Hamdu Shaka yupo wilayani Bukoba kwa ziara ya siku mbili ya uimarishaji wa chama na ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM 2020-2025 ikiwa ni sehemu ya ziara ya Sekretarieti ya CCM Taifa mkoani Kagera inayoongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho Ndg Daniel Chongolo.