SERIKALI imezindua rasmi nembo na kaulimbiu ya maadhimisho ya sherehe ya miaka 60, ya Uhuru wa Tanzania bara zitakazofanyika Disemba 9, mwaka huu katika uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Saalam.

Akizungumza  na Waandishi wa Habari jana,Novemba mosi 2021,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri mkuu Sera, Uratibu, Kazi, Vijana na Ajira Jenista Mhagama,amesema  kutokana na umuhimu wa maadhimisho hayo mwaka huu serikali imeazimia kuwa na shughuli zitakazofanyika maeneo mbalimbali ya nchi.

“Lengo ni kutafakari kwa pamoja na kukumbuka tulikotoka, tulipo na tunakoelekea na hasa mafanikio tuliyopata yanayoonyesha dhahiri maendeleo ya miaka 60, ya uhuru wa nchi yetu na watu wake,”amesema.

Amesema  shughuli za maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru zitahusisha Wizara na Taasisi zote za serikali kuelezea hatua ambazo kila sekta imepiga tangu Uhuru, tuliposasa na tunapoelekea.

Waziri huyo amesema ratiba ya mikutano ya Mawaziri na vyombo vya habari kuhusu historia ya nchi  tangu ilipotoka  uhuru hadi sasa kwa kila sekta itaanza Novemba  2, Novemba 2021,ambapo amedai  mikutano hiyo inaratibiwa na Idara ya Habari – MAELEZO kwa kushirikiana na sekta husika 2021.

Pia amesema  kutakuwa na mahojiano maalum kati ya vyombo vya habari na viongozi mbalimbali wa serikali walioko madarakani na wastaafu, watu mashuhuri, sekta binafsi na wananchi.