Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezindua “Ajira Portal Mobile App” itakayotumiwa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuendesha mchakato wa ajira Serikalini ambao utaondoa vitendo vya rushwa na upendeleo kwa waombaji wa ajira.

Akizindua portal hiyo jana jijini Dodoma, Mhe. Mchengerwa amesema portal hiyo itasaidia kuwapata watumishi wenye sifa stahiki na wazalendo watakaolitumikia taifa kwa weledi, uadilifu na wataolifikisha taifa kwenye uchumi wa kati wa juu.

Mhe. Mchengerwa amesema, mfumo huo wa maombi ya kazi kupitia simu ya kiganjani umelenga kuwapunguzia adha mbalimbali walizokuwa wakikutana nazo waombaji wa fursa za ajira ikiwemo upatikanaji wa taarifa zinazohusu ajira serikalini na mchakato wake.

“Mfumo huu ukitumika vizuri, ninaamini waombaji wa ajira wataweza kufanya maombi ya ajira popote walipo mijini na vijijini, kwani mfumo unamuarifu muombaji uwepo wa nafasi.

Mhe. Mchengerwa amewahamasisha waombaji wa ajira serikalini kuanza kutumia mfumo huo ambao utapunguza changamoto nyingi walizokuwa wakikabiliana nazo kabla ya uwepo wa mfumo huo.

Akimkaribisha Mhe. Mchengerwa kuzungumza na Watendaji na wadau wa ajira, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameipongeza Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa kutekeleza maelekezo ya Mhe. Mchengerwa ya kuwataka kuanzisha mfumo utakaorahisisha mchakato wa ajira kwa waombaji wa ajira serikalini.

“Nakumbuka katika kikao chako cha kwanza uliporipoti ofisini, ulikuwa na maono ya kufanya mchakato wa ajira kuwa wa kidijitali na kuelekeza mfumo huo uundwe ili kurahisisha mchakato wa ajira Serikalini, na hatimaye leo unazindua rasmi mfumo huo,” Mhe. Ndejembi ameongeza.

Aidha, Mhe. Ndejembi amesema maono ya Mhe. Mchengerwa yanaenda sambamba na utekelezaji wa azma ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akisisitiza mara kwa mara kufanya maboresho ya utoaji wa huduma katika taasisi za umma kupitia TEHAMA.

Akitoa neno la utangulizi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema kukamilika kwa mfumo huo wa Ajira App ni hatua kubwa iliyofikiwa na ofisi katika kurahisisha mchakato wa ajira serikalini kwa kutumia TEHAMA.

Ili kuhakikisha Sekretarieti ya Ajira inautumia mfumo huo ipasavyo, Dkt. Ndumbaro ameiomba Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma iliyozinduliwa hivi karibuni kushirikiana na watendaji wa Sekretarieti ya Ajira katika usimamizi wa mfumo huo ili uwe na manufaa kwa umma.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Exavier Daudi amesema huduma hiyo ya Mobile App itaongeza wigo wa upashanaji habari za ajira na kuokoa fedha ambazo waombaji walikuwa wakizitumia kulipia huduma za mtandao kwa wafanyabiashara wa huduma hizo.