Na Waandishi wetu, Dar

Serikali ya Tanzania imezihakikishia kampuni za Uswisi mazingira salama ya biashara na uwekezaji nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipokutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Daanzi katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi Mulamula amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita imetilia mkazo katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kupitia sheria na kuondoa baadhi ya kodi zilizokuwa ni kikwazo kwa wawekezaji.

“Serikali imepitia sheria zetu na kuweza kuondoa kodi zilizokuwa kero…………na kupitia pia sheria ya uwekezaji kwa lengo la kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini,” amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi pamoja na ujumbe wake wameoneshwa kuridhishwa na juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na kuahidi kuendelea kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uswisi kuja kuwekeza Tanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Daanzi amesema pamoja na mambo mengine, wamejadiliana mazingira ya biashara na uwekezaji na vitu ambavyo kampuni za Uswisi zinahitaji ili kuwekeza zaidi Tanzania.

“Tumeridhishwa na juhudi za Serikali ya Tanzania za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na tumemhakikishia Waziri Mulamula kuwa tutaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara kutoka Uswisi kuja kuwekeza Tanzania,” amesema Bi. Daanzi

Bi. Daanzi ameongeza kuwa mbali na kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji pia kuna maeneo ya ushirikiano ambayo Serikali ya Uswisi itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha maisha ya watanzania.

Katika tukio jingine, Balozi Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China Nchini Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Viongozi hao pamoja na mambo mengine, wamejadili kuhusu Mkutano wa nane (8) wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 – 30 Jijini Dakar nchini Senegal.

Katika Mkutano huo Rais wa China Mhe.  Xi Jinpign anatarajiwa kuhutubia kwa njia ya Mtandao ambapo Tanzania itawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.

Mkutano huo utawajumuisha viongozi na wawakilishi kutoka Bara la Afrika na China ambapo utatoa fursa ya viongozi hao kujadili na kuangalia jinsi ambavyo China ilivyotekeleza hatua za ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitatu 2018 – 2021 kwenye  maeneo ya ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda barani Afrika, ujenzi wa miundombinu ya nishati, usafirishaji, habari na mawasiliano, kukuza wigo wa biashara kati ya China na mataifa ya Afrika.

Maeneo mengine ni kampeni ya mapinduzi ya kijani, mpango maalum wa mafunzo ya ufundi, kuboresha sekta ya Afya, ulinzi na usalama na ushirikiano katika masuala ya habari, utamaduni sanaa na michezo.