Bei ya mafuta ya dizeli imeshuka kwa Sh18 kwa lita katika Bandari ya Dar es Salamu kutoka Sh2, 261 kwa mwezi Oktoba na kufikia Sh2, 243 kwa lita moja mwezi huu huku bei ya petroli ikibaki sawa na ya mwezi uliopita.

Akitangaza kushuka kwa bei ya dizeli jana jijini Arusha, kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Mhandisi Godfrey Chibulunje amesema mafuta hayo yameshuka kutokana na jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa bei nafuu licha ya soko la dunia kupanda.

"Katika soko la dunia bei zinazidi kupanda lakini Serikali imefanya juhudi mbalimbali za kufuta tozo na imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na soko la dunia katika upandaji wa bei za mafuta hivyo Serikali inajali wananchi wake,"amesema Chibulunje.

Amesema kuwa bei hiyo ya dizeli itaanza kutumika leo (Jumatano) na kusisitiza bei ya petroli kuwa hivyo hivyo kama awali ya Sh2, 439 kwa lita moja.

Amesema bei ya  mafuta ya taa katika bandari ya Dar es Salaam itaendelea kuwa Sh2,188 kwa lita moja na katika Bandari ya Tanga bei ya mafuta ya petroli ilikuwa ni Sh2,478 huku dizeli iliyokuwa inauzwa Sh2,245  kwa lita moja na zitaendelea kubaki hivyo hivyo.

Amekatika Bandari ya Mtwara bei itabaki kama ilivyokuwa ambapo petroli itakuwa ni Sh2, 455 na dizeli Sh2, 279 huku bei ya mafuta ya taa ikiwa ni Sh2, 260 kwa lita moja.

Amesisitiza bei ya mafuta ya petroli itakabaki hivyo hivyo na Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kudhibiti upandaji wa bei za bidhaa hizo.