Na. James K. Mwanamyoto-Arusha
Serikali imesisitiza kutowarejesha kwenye Utumishi wa Umma Watumishi 15,538 walioondolewa kazini kwa kughushi vyeti au kutoa taarifa za uongo katika kumbukumbu zao rasmi za kiutumishi kuwa wana elimu ya kidato cha nne.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jana jijini Arusha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, msimamo wa Serikali wa kutowarejesha watumishi hao waliobainika kughushi vyeti uko palepale.

“Ninasisitiza kuwa, hakuna msamaha wowote uliotolewa na Serikali kuwarejesha watumishi waliokosa uadilifu kwa kughushi vyeti au kutoa taarifa za kiutumishi zisizo sahihi,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.

Aidha, Mhe. Mchengerwa ameuarifu umma kuwa, Serikali imewaondoa pia watumishi hewa 19,708, hivyo kuiwezesha Serikali kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 19 ambazo zinatumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Akizungumzia watumishi waliorejeshwa kazini baada ya kuondolewa kwenye Orodha ya Malipo ya Mishahara, Mhe. Mchengerwa amesema, mwaka 2004 Serikali ilitoa Waraka uliobainisha kwamba watumishi wote watakaoajiriwa kuanzia tarehe 20 Mei, 2004 walitakiwa kuwa na elimu ya Kidato cha Nne ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya Sera ya Ajira na Menejimenti ya Utumishi wa Umma pamoja na Kanuni za Utumishi wa Umma.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, katika utekelezaji wa matakwa hayo, mwaka 2017 wakati wa zoezi la uhakiki wa vyeti na watumishi hewa ilibainika baadhi ya watumishi wenye elimu ya Darasa la Saba waliajiriwa bila ya kuwa na cheti cha ufaulu wa elimu ya Kidato cha Nne. Hivyo, watumishi hawa waliondolewa kazini kutokana na kukosa sifa kwa mujibu wa Miundo ya Utumishi ya Kada zao.

Amesema katika zoezi hilo, baadhi ya Waajiri waliwaondoa kwenye Orodha ya Malipo ya Mishahara kimakosa watumishi wasiokuwa na elimu ya Kidato cha Nne walioajiriwa kabla ya tarehe 20 Mei, 2004. Kutokana na makosa hayo, mwaka 2018 Serikali kupitia Waajiri na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora iliwarejesha kazini na kuendelea kuwalipa mishahara jumla ya watumishi 4,380 walioondolewa kwenye Orodha ya Malipo ya Mishahara kimakosa. Idadi hii inajumuisha Watendaji wa Kata, Watendaji wa Mtaa na Watendaji wa Kijiji wapatao 3,114.

Pamoja na kuwarejesha watumishi tajwa, Mhe. Mchengerwa amesema Serikali pia ilitoa msamaha wa kuwarejesha kazini watumishi walioondolewa kazini kwa kukosa sifa ya elimu ya Kidato cha Nne na baadaye wakajiendeleza na kupata sifa tajwa hadi kufikia mwezi Desemba, 2020. Msamaha huu uliwahusu watumishi waliojipatia vyeti vya elimu ya Kidato cha Nne ambao hawakudanganya katika taarifa zao kuwa wana elimu ya Kidato cha Nne au hawakubainika kughushi vyeti.

Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Mchengerwa kuzungumza na Waandishi wa Habari, Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema lengo la Mhe. Mchengerwa kuzungumza na Vyombo vya Habari ni kutoa ufafanuzi juu ya upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya mitandao ya kijamii kuwa Serikali imeamua kuwarejesha kazini watumishi walioghushi vyeti na walioajiriwa kwa cheti cha darasa la saba ambao walishindwa kujiendeleza ili kupata sifa stahiki hadi kufikia mwezi Desemba, 2020 kama Serikali ilivyoelekeza.

Ameongeza kuwa, Ofisi yake iliwaandikia waajiri wote barua tarehe 7 Mei, 2021 kuelekeza namna ya kuhitimisha suala la hilo ambalo waathirika wamekuwa wakiibua hoja nyingi ambazo tayari Serikali ilishazitolea maamuzi.

Dkt. Ndumbaro amesema upotoshwaji unaendelea kufanywa licha ya Mhe. Waziri Mkuu, Msemaji wa Serikali na Mhe. Mchengerwa mwenyewe kutoa ufafanuzi wa suala hili hivi karibuni, hivyo Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma ameona ni vema akazungumza tena na Vyombo vya Habari ili kulielezea kwa kina suala hili na hatimaye jamii ielewe hatua zilizochukuliwa na Serikali na msimamo wake.