Na Saidina Msangi, Dar es Salaam
Serikali imetoa wito kwa wadau wa maendeleo kuisaidia katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/22-2025/26 utakao gharimu jumla ya Sh. trilioni 114.9.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba alipokuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili wa Majadiliano ya Kimkakati kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo, jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa mkutano huo utawezesha upatikanaji wa michango ya wadau ili kuboresha sera na miongozo mbalimbali ili kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano pamoja na maandalizi ya mwongozo wa uandaaji wa mipango na bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/23.
“Mkutano hu utatoa fursa kwa Wadau wa Maendeleo kuona maeneo wanayoweza kuchangia hasa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano katika miradi wanayoweza kuchangia,”alisema Bw. Tutaba.
Alitoa wito kwa wadau wa maendeleo wanaochangia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini kutoa ahadi zao mapema katika kuchangia bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 ili kuiwezesha Serikali kuandaa bajeti halisi.
Alisema maandalizi ya bajeti yatatokana na mazungumzo ya mkutano huo ambapo sekta mbalimbali zinatarajiwa kuwasilisha zilivyojiandaa katika taasisi zao, changamoto zilizojitokeza na mapendekezo ambayo Serikali itayaingiza kwenye bajeti.
Alisema Serikali inaendelea kujenga mazingira wezeshi ikiwemo sera imara, kupunguza urasimu kuvutia sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa kuchangia kiasi cha Sh. trilioni 40.6 na Serikali kuchangia kiasi cha Sh. trilioni 74.3.
“Tunakaribisha sekta binafsi kushiriki katika miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo utekelezaji wa miradi iliyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa, mradi wa ujenzi wa reli ya mwendo kasi pamoja na kuimarisha utendaji wa Shirika la Ndege nchini-ATCL ,”alisema Bw. Tutuba.
Aidha, Bw. Tutuba alizielekeza taasisi za elimu na utafiti nchini kufanya tafiti zitakazoiwezesha Serikali kuboresha utoaji wa huduma na hasa maeneo yanayoweza kuibua vyanzo vipya vya kodi ili kuchangia bajeti ya Serikali.
Mkutano huo wa siku mbili uliohudhuriwa na makatibu wakuu, wadau wa maendeleo, asasi za kiraia, sekta binafsi pamoja na maafisa wa serikali nchini kwa mara ya kwanza umeshirikisha asasi za kiraia na Sekta Binafsi kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo nchini.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi na Mratibu wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti mwenza wa Washirika wa Maendeleo Nchini Bw. Zlatan Milisic ameipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali za kuleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi nchini.
Bw. Milisic amepongeza hatua ya Serikali kuruhusu wanafunzi wanaopata ujauzito kuruhusiwa kurudi shuleni kuendelea na masomo kwa mfumo wa kawaida na kuahidi kuwa wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Sekta ya Binafsi Nchini Bw. Andrew Mahiga alisema kuwa Sekta binafsi nchini iko tayari kushirikiana na Serikali kutekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa na kuwa itachangia kuwekeza katika sekta za kilimo, mifugo, Tehama na uchumi wa bluu kwa kuwekeza na kushauri masuala ya sera ili kufikia malengo yaliyopangwa na Serikali.
Bw. Mahiga ameishukuru Serikali kwa kuijumuisha sekta binafsi katika mkutano huo muhimu kwa maendeleo ya nchi na namna inavyoendelea kuishirikisha katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo na kupokea maoni yao.