Na Mwandishi wetu
SERIKALI imejipanga kuhakikisha inaokoa takribani nusu trilioni ya fedha ambazo zimekuwa zikienda nje kila mwaka kwa ajili ya kuagiza mafuta ya kupikia kwa kuja na mbegu za kisasa, kuboresha shughuli za ugani pamoja na tafiti ili kujitosheleza.

Akifungua kongamano linalojadili sera za namna Tanzania inavyoweza kujitosheleza kwa mafuta ya kupikia mkoani Dar es Salaam jana, Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda alisema kiasi hicho kikiokolewa, kitasaidia katika kuchangia uchumi wa ndani na kutengeneza ajira zaidi kwa vijana.

“Tunazalisha wastani wa asilimia 45 tu ya mahitaji yetu na tunatumia wastani wa Sh bil 475 kila mwaka, karibu nusu trilioni. Unapopeleka kiasi hicho nje, unaenda pia kuboresha ajira nje. Kwa miaka mitatu tunakuwa tumepeleka nje zaidi ya fedha tulizokopa hivi karibuni IMF, Sh trilioni 1.3.

“Angalia hizo fedha za IMF zinavyofanya kazi nyingi kwa hiyo zikibaki ndani zitapunguza tatizo la ajira. Machinga wengi watakuwa wanazalisha viwanda badala ya kuwa baranarani,” alisema.

Akizungumzia kuhusu hatua zinazochukuliwa alisema ni pamoja na kusambaza mbegu bora za mazao yanayozalisha mafuta kwa wingi kama chikichi, alizeti, ufuta, karanga na nazi.

Kwa upande wa alizeti ambayo kwa sasa inaongoza kwa kuzalisha mafuta kwa wingi nchini alisema kwa sasa mkulima anapata wastani wa tani 0.7 kwa ekari wakati akitumia mbegu bora na kilimo cha kisasa anaweza kupata hadi tani 4.0 kwa ekari.

Kingine ambacho serikali imedhamiria kufanya alisema ni kuongeza bajeti ya shughuli za ugani na utafiti.

Kwa upande wa maofisa ugani alisema serikali itanunua pikipiki 2,000 ambazo zitagawiwa kwa maofisa ugani hivi karibuni, pamoja na kuwa na vifaa vya kupimia udongo na simu janja.

Waziri alisema mpaka sasa Tanzania ndio inaongoza kwa kuzalisha mafuta ya kula Afrika Mashariki na ni ya 26 duniani, Ukraine ikiongoza.

Mwenyekiti wa Chama cha Wazalisha Mafuta ya Kupikia (TASUPA), Ringo Iringo, alisema kutokana na uzalishaji mdogo, viwanda vingi vinafanya kazi kwa kipindi cha miezi mitatu hadi minne na Kufunga kwa kukosa malighafi.

Alisema Tanzania ina viwanda takribani 775 kuanzia vidogo kabisa hadi vikubwa.

Alishauri mashamba yaongezwe akisema kwani mafuta ya kupikia ni ya lazima nyumbani kuliko hata Mazao kama korosho.

Naye Mratibu wa Kitaifa wa Mazao ya Mafuta ya Kupikia kutoka Taasi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Joseph Nzunda alisema kimsingi Tanzania ina ardhi ya kutosha kuzalisha mafuta ya kula hadi kuuza nje, akisema soko ni kubwa sana.

Alisema mbegu bora kwa sasa zipo zonazoweza kuleta tija maradufu kwenye uzalishaji kinachotakiwa ni mipango bora.

Kongamano hilo limeandaliwa na wizara ya fedha na Mipango kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya-EU.