NA MUSSA YUSUPH,NYANG’WALE
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Christina Mndeme, amewahakikishia wananchi kwamba Serikali ya CCM haitofuta sera ya elimu bila malipo.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na katika kikao cha CCM Shina Namba 4, Tawi la Iseni, Kata ya Kakola, Wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita.

Alisema wananchi wanapaswa kupuuza upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu kwamba serikali itaondoa elimu bure.

“Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kupeleka mbele maendeleo ya nchi yetu, tuendelee kumuunga mkono, puuzeni maneno ya watu kwamba elimu bure itafutwa. Elimu bure haitofutwa,” aliwaeleza wananchi hao.

Alibainisha kuwa miradi yote ya mkakati, Serikali ya Rais Samia inaendelea kuitekeleza kwa lengo la kuwaondolea kero wananchi.

“Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere linaendelea kujengwa na litakapokamilika litatua changamoto ya ukosefu wa umeme, daraja la Kigongo-Busisi linaendelea kujengwa, ujenzi wa meli katika Ziwa Victoria bado unaendelea na barabara zinajengwa,” alisema.

Akizungumzia usambazaji umeme katika vijiji vya wilaya hiyo, aliagiza mchakato wa kumpata mkandarasi mpya ufanyike haraka kwani wananchi wanahitaji nishati hiyo.

“Kama mkandarasi wa kwanza mmeona hafai hakikisheni mnamtafuta mwingine haraka na mumsimamie vizuri, hakuna sababu ya kucheka na mkandarasi ambaye hatimizi wajibu wake,” alisisitiza Naibu Katibu Mkuu CCM Tanzania Bara.

Kuhusu changamoto ya upatikanaji maji, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, amemuagiza Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), Wilaya ya Nyang’wale, Mhandisi Moses Mwampungu, kuhakikisha ndani ya wiki mbili mabomba yaletwe ili kukamilisha usambazaji maji katika Kata ya Ikola.

Aidha, alimuagiza kujenga vituo sita vya kuchotea maji badala ya vituo vitatu vilivyokadiriwa ili kuwawezesha wananchi kutotembea umbali mrefu.

Mndeme alitoa agizo hilo baada ya kero hiyo kuibuliwa katika kikao hicho cha shina kwamba bado wanachangamoto ya uhaba wa maji ambapo wanalazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

“Haiwezekani mabomba hadi Desemba ndio yafike hapa. Chama kinakuagiza ndani ya wiki mbili mabomba yawe yameshafika na wananchi waanze kusambaziwa huduma ya maji,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mhandisi Mwampungu alieleza kuwa kampuni ya Simba Plastic ndio iliyoshinda zabuni ya kuleta mabomba hayo ambayo hadi Desemba mwaka huu yatakuwa yameshawasiri.

Kuhusu mashina, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Tanzania Bara, alisema CCM kimedhamiria kuimarisha uhai wa mashina.

Aliwataka viongozi wa mashina nchini kusimamia hitaji la Katiba ya CCM inayotaka kuitishwa vikao vya ngazi hiyo.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya CCM inasema kikao cha uongozi wa shina kinapaswa kufanyika kwa mwezi mara moja na mkutano wa wanachama wa shina unapaswa kufanyika mara moja kila baada ya miezi mitatu.