Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Butamo Philip anatarajiwa kuanza kusikiliza rufaa ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili.

Akizungumza na waandishi wa habari  Novemba 16, 2021, Wakili Edmund Ngemela anayemwakilisha mleta rufaa wa pili, Sylvester Nyegu amesema rufaa hiyo imepangwa kutajwa Desemba 13 mwaka huu mbele ya Jaji Philip.

Amesema rufaa hiyo namba 129, 2021 imetokana na shauri la jinai namba 105 la mwaka huu, ambapo mshitakiwa mwingine katika shauri hilo alikuwa ni Daniel Mbura.

Sabaya na wenzake wawili walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja, Oktoba 15 mwaka huu baada ya kukutwa na hatia katika makosa matatu likiwamo unyang'anyi wa kutumia silaha.

Wakati rufaa hiyo ikisubiriwa kuanza kusikilizwa, Sabaya na wenzake sita wanakabiliwa na kesi nyingine ya uhujumu uchumi inayoendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha