Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
JESHI la Polisi, mkoani Pwani limefanikiwa kupata silaha 24 zilizokuwa zikimilikiwa kinyume cha sheria baada ya wamiliki kuzisalimisha kwenye vituo mbalimbali vya Polisi.

Aidha Jeshi hilo linawashikilia watu 21 wakiwemo wanawake watatu na wanaume 18 wanaotuhumiwa kujihusisha na matukio ya uvunjaji na wizi nyakati za usiku.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Kibaha ,Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani ACP Wankyo Nyigesa alisema silaha hizo zimesalimishwa mwezi huu wa Novemba mwaka huu.

Alielezea kwamba, silaha zilizosalimishwa ni rifle mbili na risasi 40, bastola moja na risasi saba na gobore 21.

Anawaomba wananchi wanaomiliki silaha hizo kinyume cha sheria waendelee kuzisalimisha kwa hiyari kwani baada ya hapo atakayekamatwa akimiliki bila ya kibali hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Wankyo alibainisha, silaha hizi zilisalimishwa katika kituo cha Polisi Bagamoyo, kituo cha Polisi Chalinze ambapo zimebaki siku saba ili zoezi la kusalimisha kwa hiyari kwisha.

"Zoezi hilo la kusalimisha silaha kwa wanaomiliki kinyume cha sheria kuzisalimisha bila ya kuchukuliwa hatua lilitangazwa Oktoba 30 mwaka huu lilitangazwa na Waziri wa Mambo ya Ndani George Simbachawene na lilianza Novemba Mosi na litakwisha Novemba 30"alifafanua Wankyo.

Katika hatua nyingine, Jeshi hilo linawashikilia watu 21 wakiwemo wanawake watatu na wanaume 18 wanaotuhumiwa kujihusisha na matukio ya uvunjaji na wizi nyakari za usiku.

Aidha alisema kuwa watu hao walikamatwa wakati wa operesheni na misako iliyofanyika mwezi huu Novemba ili kudhibiti makosa mbalimbali ya jinai.

Kamanda huyo alitoa rai kwa wananchi wote waliovunjiwa na kuibiwa kufika katika kituo cha Polisi Kibaha Mji kutambua mali zao.