Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezindua mashine ya kupima magonjwa mbalimbali (MRI) katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC) leo Alhamisi Oktoba 18, 2021.
Rais Samia amezindua mashine hiyo baada ya kuwasili leo jijini Mwanza kuhudhuria Jubilee ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Bugando iliyoanzishwa mwaka 1971.
Baada ya kufika hospitalini hapo Rais Samia amepewa taarifa ya miradi mbalimbali inayoendelea hospitalini hapo ukiwemo mradi wa jengo la saratani ambalo Serikali ilitoa zaidi ya Sh1 bilioni.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa BMC, Dk Fabian Massaga, jengo hilo la huduma za saratani litagharimu zaidi ya Sh5.2 bilioni ambalo litakuwa na chumba maalumu cha kufanya utafiti kwa wagonjwa wa saratani kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na kwingineko.
Dk Massaga pia ametoa taarifa kwa Rais Samia juu ya mradi wa jengo la mama na mtoto ambapo mpaka ujenzi wake ukamilike litagharimu zaidi ya Sh6.5 bilioni ambapo kwa sasa hospitali hiyo imetenga Sh500 milioni ya mapato ya ndani kuanza ujenzi huo.
Amesema pia hospitali hiyo inatekeleza ujenzi wa jengo la kuhudumia wagonjwa wenye matatizo ya macho, jengo kwa ajili ya wagonjwa wa nnje na wanafanya utafiti kuhusiana na magonjwa yasiyoambukiza.