WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto na kuzitoa bila malipo ili kupunguza vifo vya akinamama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan inaonekana wazi katika kuimarisha huduma ya mama na mtoto. Tunajenga Vituo vya afya ambavyo vimewekwa miundombinu muhimu katika kutoa huduma ikiwemo jengo la mama na mtoto na chumba cha upasuaji.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumatano. Novemba 17, 2021) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Kisayansi wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mtoto, Vijana na Lishe unaofanyika mkoani Dar es Salaam. Mheshimiwa Majaliwa amefungua mkutano huo kwa niaba ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

“Mtakumbuka kuwa mwezi Novemba mwaka 2018 Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wakati akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, alizindua Kampeni ya “Jiongeze Tuwavushe Salama” ambayo ilikuwa na nia ya kuongeza uwajibikaji katika kuhakikisha mama mjamzito na mtoto mchanga wanakuwa salama.”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuielekeza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee wa Watoto ifanye mapitio ya mwongozo wa uendeshaji wa Vituo vya Afya kuhusu upatikanaji wa watumishi ili Madaktari Bingwa wapatikane hadi ngazi ya Wilaya.

“Wizara ya Elimu ihakikishe mitaala na shule zetu zinawekeza katika kufundisha somo la uzazi kulingana na umri wa wanafunzi.  Pia Mamlaka za Serikali za Mitaa zisimamie mpango wa lishe kwa wanafunzi wa shule za kutwa. Lishe ni muhimu sana katika suala zima la kuimarisha afya ya uzazi.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameielekeza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau wote kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa ajili ya watoto wachanga ikiwa ni pamoja na uwepo wa vyumba maalum kwa ajili ya watoto wachanga wagonjwa, vifaa tiba na watoa huduma wenye ujuzi.

“Wadau wote katika ngazi zote, kuwekeza ipasavyo kwenye mifumo ya huduma za afya ya uzazi na mtoto ili tufikie malengo endelevu ifikapo 2030, ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi hadi 70 kwa kila vizazi hai 100,000 na vifo vya watoto wachanga kufikia 12 kwa kila vizazi hai 1,000.”  

Kwa upande wake, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amesema uzazi wa mpango ni afua muhimu katika upunguzaji wa vifo vitokanavyo na uzazi na unasaidia  katika kuboresha afya ya mama na kumfanya ashiriki vema katika ujenzi wa Taifa na kuongeza kipato kwa familia.

“Uzazi wa mpango unasaidia kumpa mama nafasi ya kumnyonyesha motto wake angalau kwa miaka miwili kama inavyoshauriwa kiafya. Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeendelea kuwekeza na kutoa huduma kwenye afua hii na kwa sasa matumizi ya uzazi wa mpango kwa takwimu za ndani unafikia asilimia 39 tukiwa na lengo la kitaifa la kufika asilimia 47 ifikapo mwaka 2023.”

Amesema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye upatikanaji wa huduma za dharura za afya ya uzazi na mtoto mchanga hapa nchini kwa kujenga na kuweka vifaa tiba vya kuwezesha kutoa huduma za dharura za uzazi na mtoto, kutoa dawa ya ganzi/usingizi na kufanya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni.

Dkt. Gwajima amesema Tanzania ina jumla ya vituo vya afya 911 na kati yake vituo 491 sawa na asilimia 51 vinatoa huduma za dharura za uzazi na mtoto timilifu ikiwa ni pamoja na upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni.

“Vituo hivi vipya vimeanza kufanya kazi baada ya kuhakikisha kuwa vinapata watumishi stahiki ikiwa ni pamoja na watumishi waliopata mafunzo ya kutoa dawa za ganzi na usingizi katika shule za MUHAS, KCMC na Bugando.”

Naye, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amesema Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Hussein Mwinyi imeweka mikakati thabiti katika kuhakikisha inapunguza vifo vya mama na mtoto na hiyo imechangiwa na uboreshaji mkubwa wa huduma za afya kuanzia ngazi ya chini.