Serikali imeahidi kukamilisha ujenzi wa jengo la kuhifadhia mashine za kutoa tiba ya mionzi kwa ajili ya matibabu ya saratani, kufuatia uhitaji wa haraka wa mashine hizo.

Ahadi hiyo imetolewa mkoani Mwanza na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa hospitali ya Bugando.

Ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa jitihada wanazozifanya katika utoaji wa huduma, huku akisema kuwa tiba ni muhimu.

“Tiba ni sadaka, ukiweza kumrudishia mtu afya yake, ukamtibu akaendelea na kazi zake ni sadaka kubwa,” amesema Rais Samia Suluhu Hassan.

Ameelekeza kufanyika kwa uchunguzi ili kubaini kiini cha kuwepo kwa wimbi kubwa la saratani Kanda ya Ziwa, ambapo wengi wa wagonjwa hao wamekuwa wakihudumiwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road iliyopo mkoani Dar es Salaam.

“Waathirika wengi wa saratani wakiwa ni Wanawake wanaoshambuliwa zaidi na saratani za kizazi na matiti,  mfanye utafiti kubaini chanzo cha saratani hizo na kwanini wakazi wa Kanda ya Ziwa ndio waathirika wakubwa,” ameelekeza Rais Samia Suluhu Hassan.

Kila mwaka Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya mahitaji mbalimbali kwenye hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.