Rais Vladimir Putin wa Russia amesema katika hotuba yake mbele ya kundi la G20 kwamba makombora ya Marekani yaliyoko barani Ulaya ni tishio kwa usalama wa nchi yake.

Shirika la habari la Sputnik limemnukuu Vladimir Putin akisema hayo katika kikao cha maafisa wa wizara ya ulinzi na mawakala wa viwanda vya kijeshi na kuongeza kuwa, Marekani ina nia ya kuweka makombora yake ya masafa ya kati barani Ulaya na kwamba mpango huo wote ni hatari na ni tishio kubwa kwa usalama wa Russia. 

Amesema, mfumo wa Russia wa kujilinda mbele ya mashambulizi ya anga ya aina yoyote ile unabidi uwe na uwezo wa kutungua makombora yenye kazi kubwa kuliko sauti tena ya aina yoyote ile.

Kabla ya hapo pia rais huyo wa Russia aliwahi kuonya kwamba kama Marekani itaweka makombora mapya ya nyuklia barani Ulaya, Russia nayo haitokaa kimya, bali itachukua hatua madhubuti za kukabiliana na uchokozi huo.

Alisema, nchi yoyote ya Ulaya ambayo itakubali kuwekewa makombora ya Marekani, ijue kuwa haitosalimika na mashambulizi ya Russia, kwani Moscow inaihesabu sehemu yoyote yenye silaha zinazohatarisha usalama wake, sehemu hiyo ni ya adui na ina haki ya kujihami.

Mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu pia, Rais Vladimir Putin wa Russia alielezea wasiwasi wake kuhusu mpango wa Marekani wa kuweka mifumo yake ya kujilinda kwa makombora katika mpaka wa Russia na Japan na aliitaka Tokyo isiruhusu kufanyika jambo hilo. 

Aidha aliitaka Japan itoe uhakikisho wa kutiwa saini makubaliano ya amani baina ya Tokyo na Moscow. Ikumbukwe kuwa Russia na japan zina mgogoro wa visiwa vya Kuril ambavyo vilitekwa na Umoja wa Kisovieti mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia na hicho ni kikwazo cha kutiwa saini makubaliano ya amani baina ya Russia na Japan.

-Parstoday