Na. A/INSP Frank Lukwaro- Jeshi la Polisi.

Mkutano wa Maafisa Wanandhimu, Wakuu wa Usalama barabarani na Wahasibu wa Polisi kutoka mikoa yote Tanzania bara na Zanzibar wametakiwa kuongeza kasi katika kukusanya maduhuli ya serikali ikiwemo kuwasimia walio chini yao ili kuepusha hoja za kiukaguzi ambazo zinaweza kujitokeza kutokana na usimamizi usioridhisha kwa baadhi ya Viongozi.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Fedha na Lojistiki Hamad Hamis Hamad wakati wa siku ya pili ya mkutano huo unaoendelea Mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kuboresha utendaji kazi kwa washiriki hao pamoja na kujiimarisha katika utumiaji mifumo ya kidigitali katika kukusanya mapato ya serikali ikiwemo tozo za barabarani.

Amesema ni vizuri washiriki wa mkutano huo kuhakikisha kuwa mkutano huo utakapomalizika mabadiliko yaweze kuonekana kwa vitendo kwakuwa kila mmoja anatakiwa kutambua wajibu wake katika kuhakikisha kuwa mapato ya Serikali yanakusanywa na kufikishwa katika mamlaka husika kwa wakati.

“Kila mmoja aone umuhimu wa kuongeza bidii katika ukusanyaji wa mapato na kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha na rasilimali za umma ili kufikia malengo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” Alisema Kamishna Hamad.

Mkutano huo pia umeshirikisha wadau wa nje wakiwemo Wizara ya Fedha na Mipango, Mamlaka ya udhibiti wa Ardhini (LATRA), Ofisi ya Mhakiki mali wa Serikali ambapo wameweza kuwasilisha mada zao na kufanya majadiliano ya pamoja ili kuboresha ushirikiano uliopo baina ya taasisi hizo na Serikali.

Vilevile Wajumbe hao wameweza kuelimishwa kuhusu ufanyaji kazi wa mashine mpya za ukusanyaji wa tozo za serikali (POS) ambapo zimeboreshwa katika ufanyanyaji wa kazi ambapo jumla ya mashine hizo 2,050 zimenunuliwa ili kuendeleza zoezi hilo la ukusanyaji wa tozo hususani za barabarani.

Mkutano huo ulifunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na unatarajia kufungwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini unabebwa na kauli mbiu ya Kusanya mapato, Simamia fedha na mal iza Umma kwa maendeleo ya Taifa.