Na Munir Shemweta, MISENYI
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuendelea kuwekeza miradi ya kimkakati itakayoliwezesha shirika kujiongezea kipato.

Dkt Mabula ametoa kauli hiyo tarehe 23 Novemba 2021 wakati akikagua mradi wa jengo la kibiashara la NHC lilipo mpakani mwa Tanzania na Uganda eneo la Mutukula wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.

Naibu Waziri ambaye alikuwa katika  ziara ya siku mbili mkoani Kagera alisema, ilichofanya NHC kujenga jengo la kibiashara katika mpaka wa Tanzania na Uganda Mutukula ndicho serikali inachokitaka pale inapokuwa na taasisi zinazojitegemea katika uendeshaji pia ziwe na njia tofauti za kujiongezea kipato kitakachosaidia kuongeza miradi mingine.

" Hiki ambacho NHC mmekifanya hapa kujenga jengo la biashara Mutukula ndicho inachokitaka serikali  kuwa inapokuwa na taasisi inayojitegemea kiuendeshaji pia iwe na njia tofauti za kujiongezea kipato cha shirika " alisema Dkt Mabula.

Kwa mujibu wa Dkt Mabuka, mradi wa jengo la biashara Mutukula unatoa fursa kwa wafanyabiashra kutoka nchi jirani ya Uganda kuja Tanzania kununua bidhaa kwani awali ilikuwa aibu kuona wafanyabiashara wakienda kununua bidhaa katika maduka ya nchi hiyo.

" Ilikuwa aibu tunaenda upande wa pili kununua bidhaa lakini sasa na wao waje hapa kufanya biashara na hii ni alama tosha kuwa tunaanza kubadilika" alisema Naibu Waziri Mabula.

Aidha, Dkt Mabula aliongeza kuwa, ana imani mradi wa jengo la kibiashara Mutukula ukienda vizuri eneo lingine linalokusudiwa kujenga maduka litapata msaada wa fedha za ndani zitakazopatikana kupitia mradi huo.

Naibu Waziri Mabula aliongeza kuwa,  ni kweli wafanyabiashara wadogo wamachinga hawawezi kupanga katika jengo la mradi huo lakini shirika linaweza kujenga maduka kuzunguka jengo hilo yanayoweza kubadilisha sura ya eneo kuonesha kuwa eneo hilo limepangwa na isiwe viduka visivyoonesha tofauti kati ya eneo lilipangwa na lisilopangwa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Misenyi mkoani Kagera Projestus Tegamaisho Mutukula amelishukuru Shirika la Nyumba la Taifa kwa uamuzi wake wa kuwekeza mradi huo katika eneo la Mutukula ambapo aliiomba NHC kuangalia uwezekano wa kuwekeza mradi kama huo katika mji unaopanuka wa Bunazi wilayani Misenyi.

"Niwashukuru NHC kwa kutuwekea kitega uchumi cha jengo hili na tunaomba mtujengee jengo lingine katika mji wa Bunazi ili maeneo ya Misenyi yawe na uwelezaji mkubwa" alisema Tegamaisho.

Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Kagera Maneno Mahenge alisema, mradi wa jengo la Mutukula kwa sasa umefikia asilimia 99 na mradi huo umetumia asilimia 50 tu ya  eneo lake lenye ukubwa wa mita za mraba 7900.

" Tunataka mradi huu wa kitega uchumi hapa Mutukula uwe shopping centre area inayotembelewa na wananchi wengi wakiwemo wa nchi jirani ya Uganda na jengo hili tayari lina wapangaji 36" alisema Mahenge.

Aidha, katika kuhakikisha NHC unawekeza majengo ya kimkakati maeneo ya mipakani Meneja huyo wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Kagera alieleza kuwa, tayari amepeleka Andiko Makao Makuu ya NHC kwa ajili ya kuanzisha miradi kama wa Mutukula katika eneo la Rusumo mpaka wa Tanzania na Rwanda pamoja na Kabanga katika mpaka wa Tanzania na Burundi.