Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amefichua mbinu chafu ambayo hufanywa na wataalam wa mifugo wasio waaminifu kwa kushirikiana na baadhi ya  wasimamizi wa hifadhi za taifa ambao hushirikiana kuuza mifugo iliyoingia hifadhini kinyume na utaratibu.

Ndaki ameyasema hayo jana (03.11.2021) wakati akizindua miaka minne ya nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Veterinali kwenye kikao  kilichofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ndogo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi uliopo jengo la NBC jijini Dodoma.

“Askari wa hifadhi wanaweza kukamata mifugo 570 kisha  wanamuita daktari wetu ambaye tumemsajili na kumtaka athibitishe kwa nyaraka vifo vya ng’ombe 400 huku wengine 100 akipendekeza kuwa hawafai kutumika tena kwa afya ya mlaji halafu wale 70 ndio mfugaji anaambiwa awalipie faini ili awachukue, huku nyuma wanaenda kuuza wale ng’ombe 500 kisha wanagawana fedha” Amefafanua zaidi Ndaki.

Ndaki amewataka wataalam wote wa mifugo wanaosajiliwa na Baraza hilo kuwa waaminifu na kuwahudumia wafugaji kikamilifu ili ufugaji wao uwe na tija na uweze kutoa mchango kwenye pato la mfugaji na taifa kwa ujumla ambapo amebainisha kuwa Wizara haitamvumulia mtaalam yoyote ambaye atatekeleza wajibu wake kinyume na taratibu.

“Lakini pia Baraza ni lazima lihamasishe wafugaji kutumia wataalam waliosajiliwa kwa kuwaelimisha wafugaji umuhimu wa baraza hilo na nitumie fursa hii kuwaelekeza wafugaji kote nchini kutumia wataalam hata kama wanafuga mifugo ya asili kwa sababu imefikia hatua mfugaji anahudumia mifugo yake kwa mazoea hali inayomfanya naye ajigeuze kuwa daktari wa mifugo yake” Amesisitiza Ndaki.

Awali wakati akimkaribisha Mgeni rasmi wa kikao hicho, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Amosy Zephania amesema kuwa baraza hilo linapaswa kujifunza namna mabaraza mengine yanavyofanya kazi ili liweze kuwa na tija kwa wafugaji wakati wa utekelezaji wa majukumu yake.

“Kwa mfano hili la kuwa na vishoka, mimi naona kuna ombwe ambalo vishoka wanaliona na ndio maana wanaamua kulitumia hivyo nikuombe Mwenyekiti uliangalie kwa umakini hili kwa sababu haiwezekani pamoja na kuwa na wataalam wengi bado kunakuwa na idadi kubwa ya vishoka” Amesema Zephania.

Awali akizungumzia mafanikio ambayo baraza limeyapata chini ya miaka 8 ya uongozi wake , Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Prof. Rudovick Kazwala amesema baraza hilo limesajili jumla ya madaktari wa wanyama 381 sawa na asilimia 83 ya lengo la kusajili madaktari 460 huku likiandikisha wataalam wasaidizi 1065 ikiwa ni asilimia 26.6 ya lengo la kuandikisha wataalam 4000.

“Lakini pia Baraza limetoa leseni 858 kwa wakaguzi wa nyama, leseni 65 kwa wataalam wa maabara na leseni 74 kwa wahimilishaji huku pia tukisajili vituo vya afya ya wanyama 1832 sawa na asilimia 57.3 ya kusajili vituo 3200” Amesema Prof. Kazwala.

Akitoa neno la Shukrani kwa Mgeni rasmi wa kikao hicho, Mwenyekiti wa baraza hilo Prof. Lughano Kusiluka mbali na kumshukuru Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki kwa Imani aliyoionesha juu yake na kumteua kushika wadhifa huo ameahidi kushirikiana na wajumbe wote wa baraza hilo kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji.

“Maelekezo yako yote nimeyapokea na ninaahidi nitashirikiana na wenzangu kuhakikisha takwimu ya wingi wa mifugo iliyopo inaendana na mabadiliko ya maisha ya mfugaji na kuongeza pato la taifa kwa ujumla kwa sababu ni kweli hatuwezi kujivunia wingi wa mifugo ambao hauleti tija kwa wafugaji wetu” Amehitimisha Prof. Kusiluka.

Baraza la Veterinali nchini lilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha sheria ya Veterinali sura ya 319 ya mwaka 2003 ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo baraza hilo linapaswa kuwa na wajumbe 9 ambao huteuliwa na Waziri anayeongoza sekta ya Mifugo na wajumbe hao huwakilisha wadau mbalimbali waliopo kwenye huduma za afya ya mifugo.