Na Munir Shemweta, WANMM
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesikitishwa  na baadhi ya Makampuni yanayofanya kazi za urasimishaji makazi holela mkoa wa Dar es salaam kutuhumu watendaji wa sekta ya ardhi kuwa wanachelewesha kazi  wakati tatizo liko ndani ya makampuni yao.

Katika kikao chake na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya Manispaa ya ubungo pamoja na makampuni yanayofanya kazi ya urasimishaji makazi holela kwenye manispaa hiyo, makampuni hayo yalimueleza Naibu Waziri Dkt Mabula kuwa yanashindwa kukamilisha kazi kwa wakati kutokana na watendaji wa sekta ya ardhi kushindwa kutoa kazi za upimaji wanazopeleka ofisi za ardhi kwa wakati.

Kufuatia tuhuma hizo Dkt Mabula aliyataka makampuni hayo kufika ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dar es Salaam kuangalia mfumo wa miamala ya ardhi kwa lengo la kubaini wanaokwamisha kazi ili aweze kuchukua hatua.

Hata hivyo, wakati wa kupitia kazi za makampuni kwenye mfumo Novemba 4, 2021 ilibainika kuwepo uzembe kwa baadhi ya makampuni kwa kushindwa kufuatilia kazi zao ama kutokuwa na mawasiliano watu wanaowatuma kufuatilia kazi zilizopelekwa Wizarani.

‘’Mfumo wa sasa hivi haudanganyi kabisa na ardhi ya sasa siyo ile ya zamani hata mtu akifanya vurugu ama kutegea kufanya kazi atagundulika tu kwa kuwa kila kitu kiko katika mfumo, ninyi taarifa mmepewa tangu mwezi wa sita halafu mnailaumu wizara’ alisema Dkt Mabula.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwaeleza wawakilishi wa makampuni DIMWE Land Consult Ltd na MOSAIK Company Ltd yaliyofika ofisini  kwa Kamishna kuwa, sasa hivi ukitaka kufuatilia kazi za ardhi kupitia mfumo kuanzia mwanzo hadi mwisho utaipata na utagundia uzembe uko kwa mtendaji gani na kusisitiza kuwa, kwa sasa hakuna tena udanganyifu kama ilivyokuwa ikifanyika zamani.

Awali katika ziara yake Naibu Waziri Dkt Mabula alikagua mfumo Unganishi wa Taarifa za ardhi katika ofisi ya ardhi Manispaa ya Ubungo Dar es Salaam na kujionea utendaji kazi pamoja na changamoto zinazowakibili watendaji wa sekta ya ardhi ambapo akiwa katika ofisi hiyo aliwataka watendaji hao kuongeza kasi ya utoaji hati za ardhi.

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi alizungumza na wakazi wa Mbezi kwa Yusufu kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili kuhusiana na sekta ya ardhi sambamba na kutoa hati kwa wananchi waliorasimishiwa makazi yao ambapo hata hivyo, wengi wa wananchi katika mkutano huo walilalamikia makampuni ya urasimishaji makazi holela kwa kuchelewesha kazi huku makampuni hayo yakiwa yamechukua fedha za wananchi.