Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. Mwigulu Nchemba amesema Tanzania ina jumla ya mabilionea 5,740 sawa na asilimia 4.2 ya utajiri katika kundi la mabilionea 140,000 waliopo Barani Afrika.

Dk. Mwigulu ametoa kauli hiyo leo tarehe 4 Novemba, 2021 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Rashid Abdallah Shangazi (CCM).

Shangazi amehoji Tanzania ina idadi ya watu takribani milioni 55 wenye madaraja tofauti ya uchumi; Je, katika idadi hiyo Tanzania ina mabilionea wangapi?

Akijibu swali hilo, Nchemba amesema kutokana na utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mwaka 2014/2015 na kurejewa mwaka 2019/2020, unaonesha idadi ya mabilionea duniani inakadiriwa kufikia watu milioni 14.

“Na kwa mujibu wa ya report ya RBC Wealth management ya Julai mwaka 2019, bara la Afrika lina mabilionea 140,000 sawa na asilimia moja ya mabilionea wote duniani,” amesema.

Amesema miongoni mwa mabilionea 5,740, waliopo Tanzania, mabilionea 115 sawa na asilimia mbili ya utajiri wa dola za Marekani milioni 30, wanamiliki zaidi ya asilimia 28 ya utajiri wote wa mabilionea wanaotoka Tanzania.

“Kati ya hawa wengi wamesajiliwa TRA, na wanalipa kodi zao katika idara ya walipa kodi wakubwa. Na wamewekeza katika sekta ya viwanda, nishati, madini na wamewekza pia katika sekta ya fedha, mawasiliano, uchukuzi, utalii na makazi,” amesema.

Aidha, amesema mabionea hao wanatoka katika sekta mbalimbali kama vile madini, viwanda, mawasiliano na ujenzi na sekta nyingine ambazo hakuzitaja .