Wakili wa Mwanaume "Brenton Tarrant" aliyewauwa Waumini 51 wa Kiislamu katika shambulio baya kwenye Misikiti miwili mjini Christchurch, New Zealand, amesema mteja wake anafikiria kukata rufaa dhidi ya kifungo cha maisha alichopewa, akisema alishinikizwa kukiri makosa baada ya shambulio hilo la mwaka 2019.


Wakili huyo Tony Ellis, amesema Mteja wake amemfahamisha kuwa alikiri makosa baada ya kupitia visa vya udhalilishaji wakati akisubiri kuanza kwa kesi yake.

Ellis ameyawasilisha malalamiko hayo Mahakamani na uchunguzi umeanzishwa dhidi ya shambulizi hilo kujua iwapo mchakato unaostahili ulifuatwa katika uendeshwaji wa kesi hiyo.

Brenton Tarrant mwenye miaka 31, mwaka uliyopita alihukumiwa kifungo cha maisha bila ya uwezekano wa msamaha baada ya kukutwa na hatia ya kuwaua Waumini hao 51 wa Kiislamu na jaribio la kuwaua Waumini wengine 40 katika shambulio lililofanyika tarehe 15 mwezi Machi mwaka 2019 lililosemekana kuwa baya zaidi kuwahi kutokea nchini humo.