Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshiriki Mkutano wa ishirini na sita wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi. Mkutano huu unafanyika katika Jijini la Glasgow nchini Uingereza kuanzia tarehe 31 Oktoba mpaka tarehe 12 Novemba 2021.

Lengo la Mkutano huu ni kujadili athari zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi na kuweka Mikakati ya pamoja kama Dunia kukabiliana na athari hizi. Agenda ambazo zinatarajiwa kujadiliwana hatimaye kufikia Makubaliano ya kupambana na athari za Mabadiliko ya tabianchi ni pamoja na kuweka mikakati ya kutafuta Rasilimali Fedha kutoka nchi zilizoendelea kwenda kwa nchi zinazoendelea ambazo zinaathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi, takribani kiasi cha dola bilioni 100 kila mwaka za kupambana na changamoto ya Mabadiliko ya Tabianchi kidunia kutoka katika Mifuko ya Jamii za Kimataifa ikiwemo Global Environmental Facility (GEF), Gren Climate Fund (GCF), Adaptation Fund (AF), Least Developed Countries Fund (LDCF).

Agenda zingine zitakazojadiliwa ni pamoja na mikakati ya kuhimili athari za Mabadiliko ya tabianchi (adaptation),upunguzaji wa uzalishaji wa gesijoto (mitigation),kilimo na mabadiliko ya tabianchi, muda wa utekelezaji wa michango ya Taifa ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Nationally Determined Contributions Common Timeframes-NDC), Upatikanaji wa Masoko ya Hewa Ukaa chini ya Ibara ya 6 ya Makubaliano ya Paris (Carbon Markets) ili kuweza kupata fedha za kuchangia kwenye mfuko wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi (Adaptation Fund).

Majadiliano katika Mkutano huu pia yatahusu Mpango wa Taifa wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya tabianchi (National Adaptation Plans-NAPs), Ubadilishanaji wa Teknolojia baina ya Nchi zilizoendelea na zinazoendelea (Technology Development and Transfer), Ujengaji Uwezo (Capacity Building), Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi (Gender and Climate Change) na Tafiti na Uzalishaji wa Taarifa (Research and Systematic Observation).

Katika Mkutano huu Tanzania inashiriki kikamilifu katika majadiliano ya masuala yenye maslahi mapana kwa nchi na kuweka msimamo katika masuala ya Rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Mkataba na Makubaliano ya Paris kwa kuzitaka nchi zilizoendelea kutimiza wajibu wao wa ahadi ya kutoa fedha hizi kama ilivyokubaliwa katika mikutano iliyopita.

Katika agenda ya Kujenga Uwezo Tanzania inahimiza  nchi zilizoendelea pamoja na mashirika ya kimataifa kutilia mkazo suala la kujenga uwezo wa nchi zinazoendelea ili ziweze kutoa mchango wake kifedha, kiteknolojia na kiutaalamu katika kupunguza uzalishaji wa gesijoto duniani.

Katika nyanja ya Kilimo na Mabadiliko ya Tabianchi katika Mkutano huu unaoendelea Tanzania inasisitiza kuwa sekta ya kilimo isijumuishwe katika sekta zinazotakiwa kupunguza gesi joto kwa kuwa kilimo kinaathirika sana na athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na kutegemea mvua. Agenda hii imekuwa na maoni kinzani kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea kuhusu kujumuisha sekta ya kilimo katika sekta zinazotakiwa kupunguza uzalishaji wa gesijoto.

Masuala mengine yatakayojadiliwa ni pamoja na Uendelezaji na usambazaji wa teknolojia, Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, Upunguzaji gesijoto kwa kutumia biashara na Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano wa COP 26 una faida kubwa kwa nchi ikiwa ni pamoja na kupata rasilimali fedha na utaalamu utakaowezesha utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali ya kupunguza na kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi. Aidha, ushiriki katika mkutano huo utasaidia kufungua uwekezaji wa sekta binafsi na kuongeza miradi ya Asasi za Kiraia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Leo tarehe moja na kesho tarehe mbili mwezi huu wa kumi na moja ni siku ambazo viongozi mbalimbali duniani wakiwemo Wakuu wa Nchi watahutubia dunia kupitia Mkutano huu.