Na mwandishi wetu, Dakar
Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaanza leo tarehe 29 hadi 30 Novemba 2021 jijini Dakar nchini Senegal.

Maafisa waandamizi kutoka katika nchi za Afrika na Jamhuri ya Watu wa China wamekamilisha maandalizi  yaliyokuwa yanahitajika ya mkutano huo, kwa kupitia na kukubaliana na nyaraka za taarifa za utekelezaji wa miaka mitatu baada ya kikao cha saba katika kikao kilichofayika tarehe 28 Novemba, 2021.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine ameongoza ujumbe wa Tanzania hicho, ambacho pia kilihudhuduriwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mpango Zanzibar Dkt. Juma Akil, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bibi Amina Shaaban, Balozi wa Tanzania Nigeria ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchni Senegal Dkt. Benson Bana na Balozi Ceasar Waitara Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mkutano huo wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika, utakuwa chini ya Wenyekiti Wenza wa Rais wa Jamhuri ya Senegal Mhe. Macky Sall na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping ambao pia watahutubia wakati wa ufunguzi wake.

Mkutano huo unatarajiwa kufanya maamuzi na kutoa maelekezo kuhusu utekeleaji wa masuala ya namna ya kuendelea kukabiliana na virusi vya ugonjwa wa Korona, ushirikiano kati ya China na Afrika, Ushirikiano wa Kisiasa, Ushirikiano wa Kiuchumi, Ushirikiano wa Maendeleo ya Kijamii, Utamaduni na Ushirikiano kati ya Watu na Watu, Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama, Mapinduzi ya Kijani, Ubadilishanaji Uzoefu katika masuala ya Uongozi Bora pamoja na Maendeleo ya Kitaasisi ya Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika na mabadiliko ya tabia nchi.