Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili jumla ya miradi mikubwa ya kimkakati kwa kupewa hadhi ya miradi mahiri ipatayo 43, ambayo itatoa ajira 130,720.

Sambamba na kutoa ajira hizo kwa Watanzania, pia miradi hiyo inatarajia kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani milioni 12,278.00

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Geofrey Mwambe, alibainisha hayo jana alipokuwa akitoa taarifa ya mafanikio ya wizara hiyo katika miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Alisema miradi hiyo inahusisha sekta mbalimbali, ambazo ni kilimo, uzalishaji viwandani, majengo ya biashara, ujenzi na madini.

Alisema baadhi ya miradi iliyofanikishwa kupata hadhi ya uwekezaji kupitia NISC ni wa Mount Meru Millers, Mlimani City, Dangote Industries Limited na Mtibwa Sugar Estates Ltd.

Mingine ni Kagera Sugar Estate, Kilombero Sugar Company, Kilombero Plantations Limited (KPL), Tanga Cement Company Limited, TANCOAL Energy Limited na Goodwil Ceramics (Tz) Limited.

“Tangu serikali ilipoanza kutekeleza Sera ya Taifa ya Uwekezaji na Sheria ya Uwekezaji Tanzania, wastani wa uwekezaji unaopimwa kwa kuangalia uwiano wa uwekezaji yaani ukuzaji Rasilimali kwa Pato la Taifa umekuwa ukiongezeka,” alisema Mwambe.

Vilevile, alisema takwimu zinaonyesha uwiano wa ukuzaji rasilimali kwa Pato la Taifa umekua kutoka asilimia 14.7 mwaka 1997 hadi asilimia 39.7 mwaka 2019.