Rais wa Marekani Joe Biden ameagiza kufunguliwa kwa mapipa milioni 50 ya mafuta ya akiba kutoka hifadhi yake kuu nchini humo na kuyaingiza sokoni ili kupunguza bei ya mafuta duniani.
Kufunguliwa kwa mapipa hayo ya mafuta sio tu kwamba inalenga soko kuu la duniani, bali pia kuwapunguzia mzigo Wamarekani wanaokabiliwa na mfumuko wa bei za bidhaa kuelekea kwa sikukuu ya kutoa shukrani.
Kwa mujibu wa muungano wa wamilki wa magari nchini humo, bei ya mafuta ya petroli imeongezeka kwa asilimia 50 tofauti na mwaka mmoja uliopita.
Biden amesema kufunguliwa kwa mapipa hayo hakutatatua mara moja tatizo la mfumuko wa bei, japo italeta ahueni kidogo. Baada ya tangazo la Marekani, mataifa kadhaa duniani yakiwemo India, Uingereza na Japan pia yamesema yatafungua mapipa kutoka hifadhi zao za mafuta.