Ongezeko hili la joto linatokana na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua katika maeneo mengi ya nchi yetu kama ilivyotabiriwa awali.
Hapa nchini, vipindi vya jua la utosi hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa).
Jua la utosi huambatana na hali ya Joto kali kwa sababu uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine. Vilevile, hali ya joto kali hujitokeza zaidi kunapokuwa na upungufu wa mvua kama ilivyo katika kipindi hiki.
Katika kipindi hiki viwango vya joto vilivyoripotiwa katika maeneo mbalimbali ni vikubwa ambapo mkoa wa Kilimanjaro uliripoti kiwango cha juu cha joto kilichofikia nyuzi joto 36.4 sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.6 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Novemba.
Vilevile, kiwango cha juu cha joto katika mkoa wa Dar es salaam kimefikia nyuzi joto 33.8 sawa na ongezeko la nyuzi joto 2.2 wakati katika mkoa wa Ruvuma kimefikia nyuzi joto 34.4 sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.3. Hali kama hii imejitokeza pia katika mikoa yote nchini ambapo kiwango cha joto kimekuwa kikubwa kuliko wastani wa muda mrefu.
Vipindi vya joto kali vinatarajiwa kuendelea kujitokeza katika mwezi Novemba, 2021 na kupungua kidogo ifikapo mwezi Disemba, 2021 ambapo mtawanyiko wa mvua unatarajiwa kuongezeka sambamba na mionzi ya jua la utosi kuwa imeondoka katika maeneo ya nchi yetu.
Hivyo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kutoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa za mwenendo wa hali ya hewa zinazotolewa pamoja na kutafuta, kupata na kutumia ushauri wa wataalamu wa kisekta ili kujiepusha na madhara yanayoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa ikiwemo joto kali.