Ugomvi baina ya wapenzi katika mahusiano ni kitu cha kawaida kutokana na watu hao wawili kutoka katika malezi na mazingira tofauti ya ukuaji toka wakiwa wadogo hadi watu wazima.

Wawili hao wanapoaanza kujenga mahusiano na kukaa pamoja kama familia,kuna vitu kadhaa ambavyo kila mmoja wao huvitazama tofauti na hivyo kuleta migongano. Migongano ambayo inaweza ikarekebishika kama wenza hao watamua kuifanyia kazi na kuelewana.

1.Wivu Na Kukosa Kujiamini
Wivu unatokana na jinsi ambavyo mpenzi mmoja anavyohusiana na watu wengine wa jinsia tofauti. Inaweza ikawa marafiki,wafanyakazi wenza au wapenzi wa zamani. Vyovyote vile itakavyokuwa ni kwamba wivu unasababisha ugomvi katika mahusiano mengi.

2. Mawasiliano Finyu
Mawasiliano yanapovunjika katika mahusiano ugomvi ni kitu cha kawaida kutokea.

Mawasiliano ya kawaida kati ya wapenzi husaidia sana kutoa wasiwasi wa nyendo za mwenza wako. Huleta amani na kujenga uaminifu kwa mpenzi kwako.

3. Masuala Ya Fedha
Japokuwa fedha si msingi wa mapenzi,lakini ni kitu ambacho kinahitajika sana katika maisha ya kila siku ya kila mtu na ya familia. Na kimekuwa ni mojawapo ya vitu ambavyo wapenzi katika mahusiano au ndoa hugombana sana juu yake.

Mwenza mmoja anapokuwa mtumiaji mbaya wa fedha na mwingine siyo,huibua malalamiko na ugomvi. Baadhi ya wapenzi hasa wanawake hawataki kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mahitaji ya msingi ya nyumbani na badala yake kuwaachia mzigo mkubwa wanaume.

4. Masuala Ya Familia
Familia ya nani ianze kwanza na ipi ifuate ni tatizo kubwa katika mahusiano. Upendeleo wa upande mmoja ambao kwa asili huwa unatokea tu ni chanzo cha ugomvi ndani ya nyumba.

Mitazamo tofauti kati ya mmojawapo katika wapenzi na familia ya mwenza wake husababisha kutoelewana kwa wapenzi hao ndani ya nyumba.

5. Suala La Unyumba
Japo kuwa suala kufanya mapenzi si kila kitu kwa wapenzi ndani ya nyumba lakini linachangia sana katika kuleta ugomvi aina yao. Kufanya mapenzi kupita kiasi au mara chache kunaleta matatizo kwa wapenzi hasa ambao wana uhitaji tofauti.

Wengine wanaona kama mpenzi ambaye hahitaji kufanya mapenzi mara nyingi na mwenzake labda anauhusiano na mtu mwingine zaidi yake. Au hamvutii tena kama zamani na huenda akaanza kuangalia nje.

6. Vipaumbele Katika Maisha
Wapenzi wawili wanapokuwa na mipango na malengo tofauti ni tatizo kubwa. Watu wanapokuwa katika uhusiano ambao ni wa kuishi daima,malengo na vipaumbele vyao ni lazima vioanishwe na juhudi za kila mmoja zilenge katika kufanikisha mipango hiyo ya pamoja.

Kunapotokea kuwa kila mmoja ana malengo tofauti basi hata vipaumbele vitakuwa tofauti na hapo ndipo shida zinapoanzia.

7. Uaminifu
Uaminifu katika mahusiaono ni jambo la muhimu sana. Bila uaminifu ni ngumu sana kwa mahusiano yoyote kudumu.

Uaminifu ni kitu ambacho hujengwa kwa muda mrefu na kikipotea ni ngumu sana kukirudisha. Japo inawezekana kujenga upya uaminifu lakini huchukua muda mrefu sana.

8. Wapenzi,Marafiki Na Maisha Ya Zamani
Mojawapo ya vyanzo vya ugomvi kati ya wapenzi ni wapenzi wa zamani. Mawasiliano ya aina yoyote na wapenzi wa zamani huleta wasiwasi mkubwa kwa mpenzi wa sasa. Ni kitu ambacho wapenzi wawili wanahitaji kuongea na kupanga jinsi ya kuepukana na matatizo ambayo yanaweza kusababishwa na historia zao za maisha.

Kuepukana na hii ni vyema kuvunja uhusiano wa aina yoyote na wapenzi wa zamani labda tu kama wapenzi hao ni wazazi wenza au mnafanya kazi pamoja na ni ngumu kutokuonana au kuwasiliana.

9. Watoto
Suala la uleaji na ukuzaji wa watoto linasababisha ugomvi mara nyingi kati ya wazazi. Jinsi gani mtoto avae au shule ipi aende linapelekea wazazi wengi kugombana.

10. Kazi Za Nyumbani
Imekuwa kama utamaduni kwa waafrika kuacha kazi nyingi kama si zote za nyumbani kwa mke. Kwa Wanawake ambao wanafanya kazi pia inakuwa ngumu sana. Hili linasababisha pia ugomvi kwa wapenzi nyumbani.