WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba atoe kipaumbele wakazi wa eneo la Ngomeni katika suala la ajira kwenye kiwanda cha kuzalisha bidhaa zinazotokana na zao la mkonge cha Sisalana.
Kiwanda hicho kilichoko katika eneo la Ngomeni Mkoani Tanga ambacho NSSF ilitoa takribani shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kukifufua ikiwa ni utekezaji wa kampeni ya ujenzi wa viwanda.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Alhamisi, Novemba 18, 2021) alipotembelea kiwanda hicho ambacho kabla ya kufanyiwa maboresho kilikuwa kinazalisha tani 1.5 hadi 2.5 kwa siku ambapo kwa sasa kinazalisha tani 20 kwa siku.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kwa kuwa kiwanda hicho ambacho kipo katika kata ya Ngomeni wilayani Muheza ni vema kwa uongozi wa NSSF ukatoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi wanaozunguka eneo ili waweze kunufaika na uwepo wake.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi hao watumie uwepo wa kiwanda hicho kwa kulima zao la mkonge kwa wingi kwani wanasehemu ya uhakika ya kuuza zao hilo ambalo lina faida.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amewaagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF pamoja na Afisa Kazi wa Mkoa wa Tanga wakutane na waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho na kushirikiana nao kutatua changamoto zinazowakabili.
Kampuni ya Sisalana ilianza kazi rasmi kiwandani Machi 12, 2021 ambapo ilikuta hali ya uzalishaji ikiwa ni ya kusuasua kutokana na ukosefu wa mtaji wa kuendeshea biashara na uchakavu wa mitambo.