WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kununua mitambo mikubwa na ya kisasa ya kuchimba mabwawa itakayopelekwa katika kanda zote nchini Ili kuendelea kuboresha sekta ya umwagiliaji na kuongeza tija katika kilimo.

“Serikali itaendelea kusimamia eneo ya umwagiliaji katika sekta ya kilimo kwa kuwa inatusaidia sana, tumeshatoa fedha kwa ajili ya kununua mitambo na kuboresha iliyopo, eneo hili linatija hasa katika kipindi hiki ambacho hali ya hewa inabadilika.”

Ameyasema hayo jana (Alhamisi, Novemba 11, 2021) wakati akijibu swali la George Mwinyisongole, Mbunge wa Mbozi aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali katika kuboresha kilimo cha umwagiliaji, katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kulisimamia eneo la umwagiliaji katika sekta ya kilimo kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na kwamba fedha hizo zitatumika katika ununuzi wa mitambo mipya na kukarabati mitambo ya zamani.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inatambua huduma ya usafiri inayotolewa na waendesha pikipiki maarufu bodaboda kwa kuwa zimesaidia kupunguza tatizo la usafiri na itaendelea kuboresha huduma hiyo kwa kutoa elimu kupitia Jeshi la Polisi.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Fatma Taufiq aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kutoa mafunzo kwa waendesha bodaboda ili kuepukana na ajali za mara kwa mara zinazopoteza nguvu kazi ya Taifa.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa katika kuhakikisha waendesha bodaboda wanapata elimu, polisi huwafuata katika maeneo yao na kuwaelimisha mambo muhimu ya kuzingatia wawapo barabarani ili waweze kutoa huduma hiyo vizuri.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali itaendelea na mkakati wa kuwaelimisha vijana hao, lengo likiwa ni kuwawezesha kujua thamani ya kazi yao pamoja na kuzingatia sheria za usalama barabarani. “Wakizingatia sheria watapunguza ajali.”

Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Watanzania wajiandae kutumia fursa zitokanazo na mradi wa kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) utakaojengwa mkoani Lindi. “Mradi huu mkubwa na wa kimkakati unakuja kutengeneza fursa nyingi za kiuchumi kwa Watanzania.”

Tayari Waziri wa Nishati, January Makamba ameanzisha majadiliano baina ya Serikali na Wawekezaji wakubwa wa Kampuni za Shell, Equinor, Ophir Energy, Pavillion Energy na ExxonMobil juu ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa unaotarajia kutumia Shilingi trilioni 70.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati ajibu swali la mbunge wa Kilwa Kusini, Aliy Kasinge aliyetaka kujua kauli ya Serikali juu ya kinachoendelea katika mradi huo wa kusindika gesi asilia kuwa kimiminika.