WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kulipa umuhimu wa kipekee suala la lishe nchini ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi imara kupitia maendeleo ya viwanda.

“Maendeleo ya Taifa pamoja na mambo mengine, yanahitaji uwepo wa watu (nguvu kazi) wenye afya njema na lishe bora ili kuwawezesha kufanya kazi kwa bidii na tija. Rasilimali watu imara ndio msingi wa kuzalisha kwa tija na kupunguza umaskini. Tutaendelea kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na aina zote za utapiamlo.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Alhamisi, Novemba 18, 2021) katika Mkutano wa Saba wa Wadau wa Lishe unaofanyika kwenye Hoteli ya Tanga Beach Resort Jijini Tanga. Amesema lishe bora ndio msingi wa makuzi ya kimwili na kiakili kwa watoto na husaidia kuongeza uelewa kwa wanafunzi kuwa chanzo cha ubunifu katika kazi.

Waziri Mkuu amesema madhara yanayotokana na udumavu hayana tiba, ni ya kudumu kwa kipindi chote cha uhai wa mtoto aliyeathirika, hivyo ametoa wito kwa Watanzania wote wafuate maelekezo ya wataalam wa afya na kwa pamoja washirikiane kupambana na changamoto hiyo ya udumavu.

“Vilevile, lishe bora husaidia kuimarisha kinga na afya za watu na hivyo kuipunguzia Serikali mzigo wa gharama za matibabu kwa baadhi ya magonjwa pamoja na kuzisaidia kaya kupunguza mzigo wa gharama za matibabu au vifo miongoni mwa watoto, wanawake na watu wazima ambao ni nguvukazi.”

Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutekeleza mikakakati mbalimbali kuhusu lishe ikiwemo kuwa na mipango endelevu ya maendeleo ambayo inazingatia lishe kama moja ya vipaumbele.  Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 vimeweka bayana kuwa suala la lishe ni moja ya vipaumbele vyake mahsusi.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Ofisi ya Rais TAMISEMI iendelee kusimamia Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha zinatenga kiasi cha shilingi 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano na kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatolewa kwa wakati na kutumika katika malengo kusudiwa.

Amesema sekretarieti za mikoa pamoja na halmashauri zinatakiwa zihakikishe kuwa afua zilizoainishwa katika mpango huu zinajumuishwa katika mipango na bajeti za kila mwaka, pamoja na kutengewa fedha kwa ajili ya utekelezaji.

“Sekta binafsi ongezeni kasi katika uwekezaji wa uzalishaji wa vyakula vilivyorutubishwa pamoja na kuwekeza katika kuzalisha virutubishi nchini ili kupunguza gharama kubwa ya uagizaji wa virutubishi hivyo kutoka nje ya nchi.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ameziagiza taasisi za elimu ya juu kuimarisha utafiti katika masuala ya lishe pamoja na kuhakikisha kuwa tafiti hizo zinatumika katika kutunga sera na kuelekeza afua za kimkakati za kupambana na utapiamlo.

Amesema Serikali itaendelea kusimamia masuala ya lishe na kuweka mfumo mzuri wa uratibu katika ngazi zote kuanzia Serikali Kuu, Tawala za Mikoa na hadi ngazi za Vijiji na Mitaa. “Mfumo huo umewezesha utekelezaji bora wa programu na afua za lishe na kwa mafanikio makubwa.”

Katika mkutano huo Mheshimiwa Majaliwa amezindua Mpango wa Pili Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe pamoja na Mkakati wa Utafutaji Rasilimali Fedha, amesema mpango huo unatakiwa utekelezwe kwa mafanikio na ushirikishe sekta zote.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema suala la lishe ndio kiini cha nguvu kazi yenye tija ndani ya Taifa hasa katika kipindi hiki cha ujenzi wa uchumi wa viwanda ulio shindani.

“Mapendekezo ya kufanya Mkutano wa mwaka huu hapa Mkoani Tanga ni kuhamasisha wananchi wa mkoa huu kuongeza jitihada zaidi katika kupambana na utapiamlo na nina imani kuwa uamuzi huo utasaidia kuufanya mkoa huu kuwa kinara katika masuala ya lishe na kuwa mfano kwa mikoa mingine nchini.”

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ummy Mwalimu amesema watasimamia utekelezaji wa Mpango wa Lishe ikiwa ni pamoja na kutenga shilingi 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe pamoja na kuimarisha uratibu wa masuala ya lishe katika ngazi ya Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Awali, Waziri wa Maji Jumaa Aweso alisema atahakikisha upatikanaji wa maji safi na salama nchini unaimarika ili mpango huo wa lishe uweze kuwa endelevu na wenye kutekelezeka.