Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza wizara zote zenye dhamana ya ukuzaji ajira kuhakikisha zinaandaa programu na mikakati bora ya ukuzaji ajira ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wadau wote nchini washiriki katika utekelezaji wake ili kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amezielekeza Ofisi na Wizara zote zenye dhamana za uwekezaji na biashara zihakikishe zinashirikiana na wadau wengine hususan sekta binafsi kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kutoa fursa ya kuanzishwa kwa viwanda vitakazochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira.
ametoa maagizo hayo jana (Jumatano, Novemba 24, 2021) wakati akizindua Matokeo ya Viashiria Muhimu vya Soko la Ajira kutokana na utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2020/2021. Uzinduzi huo umefanyika katika Hotel ya Golden Tulip, Zanzibar.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa idadi ya watu walio na ajira nchini imeongezeka kutoka watu milioni 20.5 mwaka 2014 hadi kufikia watu milioni 24.1 mwaka 2020/2021, sawa na ongezeko la asilimia 17.5, ambapo kati yao wanaume ni milioni 12.4 na wanawake ni milioni 11.7.
Aidha, amesema katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali kwa upande wake itahakikisha inaongeza kasi ya kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji, utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali zenye lengo la kuwezesha nguvukazi tuliyonayo kuajiriwa na kujiajiri.
Hata hivyo, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuchambua viashiria vyote na kuhakikisha kuwa inakua na ripoti ya kina itakayowezesha maboresho mbalimbali ya kukuza ajira na uchumi nchini.
Amezipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar; Ofisi ya Taifa ya Takwimu; Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar pamoja na wadau wa maendeleo kwa kufanikisha Utafiti huo.
Amesema lengo la utafiti huo ni kupata viashiria vya taarifa za soko la ajira ambavyo vitatumika kuwezesha Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo ya nchi yetu kupanga, kuhuisha na kufuatilia utekelezaji wa sera, programu na mikakati mbalimbali ya masuala ya ajira nchini.
“Utafiti huu unaviashiria vingi muhimu vinavyohusiana na masuala ya ajira nchini. Nitoe rai kwa wadau wote kupitia taarifa hii na kushirikiana na Serikali kuandaa na kutekeleza programu za pamoja za kukuza ajira kwa wananchi wetu.”
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuielekeza Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania ihakikishe inaweka utaratibu mzuri sambamba na kusimamia taasisi za fedha na mabenki nchini ili kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya biashara na uwekezaji.
“Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Miji zihakikishe katika mipango na bajeti kipaumbele kinawekwa katika kutenga fedha na kutoa mikopo yenye masharti nafuu kutokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa vijana, wanawake na wenye Ulemavu.”
“Tawala za Mikoa na Mamlaka zote za Serikali za Mitaa hakikisheni mnatenga maeneo ya kufanyia shughuli za kiuchumi na kuyawekea miundombinu inayohitajika hususan barabara, umeme, maji ili kuwezesha biashara na uwekezaji kufanyika katika maeneo hayo hususan kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo.”
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdallah amesema utafifi huo utaiwezesha Serikali kufahamu uhalisia na kupanga shughuli za maendeleo.
Naye, Waziri waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema utafiti huo utasaidia katika uboreshaji wa mkakati wa Taifa wa kukuza ujuzi pamoja na program zake.
“Lengo la kufanya utafiti huu ni kupata viashiria muhimu vya soko la ajira nchini vitakavyotumika katika kuhuisha, kutunga, kufuatilia na kutathmini ya Sera, Mikakati na Programu za Soko la Ajira.”
“Tunategemea utafiti huu utatusaidia katika uzingatiaji wa sheria za kazi sehemu za kazi; hali ya utumikishwaji wa Watoto; hali ya hifadhi ya jamii; na hali ya ushirikishwaji wa wafanyakazi.”
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Masauni amesema wizara yao inahitaji sana taarifa za ajira kwa ajili ya uchambuzi wa sera mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kubaini michango ya sekta mbalimbali katika Pato la Taifa.
Amesema taarifa hiyo itawasaidia sana wakati huu ambao Serikali Ipo kwenye maandalizi ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2022/23 na hususan katika Halmashauri zao ambapo Serikali imeelekeza zaidi kupeleka rasilimali fedha kwenye mifuko ya vijana na wanawake kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.