Mabomu mawili yaliyoripuka leo Jumanne Novemba 16, 2021 katika mji mkuu wa Uganda, Kampala yamepelekea kufungwa bunge la nchi hiyo mbali na kuuawa watu kadhaa.

Vyombo vya habari vya kieneo na kimataifa vimetangaza habari hiyo yakiwemo magazeti la kila siku ya Daily Monitor na New Vision ya nchi hiyo ambayo yamesema kuwa, bomu moja limeripuka mkabala na Kituo Kikuu cha Polisi jijini Kampala na jingine limeripuka karibu na jengo la Bunge la Uganda.

Usalama umeimarishwa kikamilifu katika majengo ya Bunge ambapo maafisa usalama wamelizingira bunge hilo hilo na uchunguzi umeanza mara moja.

Vyombo hivyo vimetangaza pia habari ya kujeruhiwa watu kadhaa kutokana na miripuko hiyo huku gazeti la Daily Monitor likitoa ufafanuzi zaidi likisema, mripuko wa kwanza umetokeka kwenye "city square" na jingine limeripuka dakika chache baadaye katika eneo la Bunge na kupiga Jengo la Bima la Jubilee ambalo ndipo zilipo pia ofisi za Inspekta Jenerali wa Serikali.

Picha na video zilizoenea katika mitandao ya kijamii zinaonyesha moshi mzito ukiwa umetanda huku baadhi ya magari yakionekana yanateketea kwa moto.

Naibu Spika wa Bunge la Uganda, Bi Anita Among amelifunga bunge hilo na kuwataka wabunge wabakie majumbani mwao. Uamuzi huo umechukuliwa dakika chache baada ya miripuko hiyo.