Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), amesema Tanzania ni moja ya nchi kusini mwa janga la sahara ambayo inaweka mikakati ya namna ya kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi kwa kuvua kiendelevu mazao ya uvuvi yaliyopo katika Bahari ya Hindi.
Waziri Ndaki amebainisha hayo (19.11.2021) jijini Dar es Salaam mara baada ya kuhudhuria mkutano wa kimataifa kwa njia ya video, kuhusu uchumi wa buluu ambao umefanyika Mjini Maputo nchini Msumbiji na kubainisha kuwa mkutano umejadili namna nchi zinazozunguka Bahari ya Hindi na kusini mwa janga la sahara zinavyoweza kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi.
Amebainisha kuwa mkutano huo umeangalia namna nchi hizo zinavyoweza kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi kwa kuvua kiendelevu na kutoharibu mazingira hali inayoweza kusababisha mabadiliko ya tabia nchi na kusababisha madhara katika sekta ya uvuvi.
Aidha, amesema mkutano huo umejadili mambo mbalimbali kuhusu uwekezaji wa uchumi wa buluu katika nchi ambazo zinazunguka Bahari ya Hindi na kusini mwa janga la sahara ambapo amefafanua kuwa uwekezaji bado ni tatizo hasa rasilimali fedha kwa nchi zinazoendelea.
Pia ameongeza kuwa mkutano huo umeangalia uvunaji wa rasilimali za mazao ya uvuvi katika Bahari ya Hindi kiendelevu pamoja na kudhibiti uvuvi haramu kwa kuweka mikakati mbalimbali ili uchumi wa buluu uwe na manufaa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla akizungumzia mkutano huo amesema, serikali ina mpango mkubwa wa kujenga vituo vya ukuzaji viumbe maji katika Ukanda wa Pwani pamoja na vituo vingine ili kufungua fursa ya uchumi wa bahari katika ukuzaji viumbe maji.
Dkt. Madalla ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuanza kufikiria namna ya kuwekeza katika uchumi wa buluu ambao unahusisha shughuli mbalimbali zinazofanyika kwenye bahari, maziwa na mito.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei amesema ili uwekezaji katika uchumi wa buluu uwe na tija na kuonekana kwa fursa mbalimbali utafiti ni eneo muhimu katika kufikia manufaa hayo.
Amesema TAFIRI itafanya utafiti katika bahari kuu kuangalia wingi na mtawanyo wa samaki ili kufahamu ni maeneo gani ambayo wavuvi wanaweza kwenda kuvua na hata kufahamu mazao wanayoenda kuvua.
Mkutano wa kimataifa kuhusu uchumi wa buluu umefanyika Mjini Maputo nchini Msumbiji, ambapo kwa Tanzania Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) ameongoza ujumbe wa Tanzania kuhudhuria mkutano huo kwa njia ya video jijini Dar es salaam, ambapo mkutano umehusisha nchi zinazozunguka Bahari ya Hindi na kusini mwa janga la sahara.