Kansela mtarajiwa wa Ujerumani Olaf Scholz amesema leo kuwa Ujerumamni inahitaji kutangaza hatua zaidi za kupambana na ongezeko kubwa la maambukizi ya virusi vya corona na kufanikiwa kupita kipindi hiki cha msimu wa baridi. 

Scholz ameitisha mkutano wiki ijayo na mawaziri wakuu wa majimbo yote ya Ujerumani kuamua kuhusu kanuni hizo mpya. Ujerumani imetangaza jana visa vipya 50,196 katika saa 24 zilizopita, ikiwa ni mara ya kwanza kwa idadi hiyo kupindukia 50,000. 

Maambukizi na vifo vimekuwa vikipanda taratibu tangu katikati ya Oktoba, katika mripuko unaodaiwa kutokana na kiwango cha chini cha utoaji chanjo Ujerumani cha asilimia 67 tu. 

Matamshi ya Scholz yamekuja baada ya kukabiliwa na ukosoaji wa kimya chake licha ya hali ya dharura, huku wakosoaji wakisema alikuwa anaangazia zaidi jaribio la chama chake cha Social Democratic la kuunga serikali ya muungano na chama cha Kijani na cha Kiliberali - FDP kufuatia uchaguzi wa Septemba.