Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita leo Jumatano Novemba 3, 2021 imeahirishwa hadi kesho kwa kuwa Sabaya ni mgonjwa.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha jana shauri la Sabaya lilipangwa kuendelea kusikilizwa leo ambapo shahidi wa upande wa Jamhuri ambaye ni Ofisa wa Tehama wa Benki ya CRDB Kanda ya Kaskazini, Jofrey Nnko, alikuwa aendelee kutoa ushahidi.

Wakili wa utetezi Mosses Mahuna aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi kesho Alhamisi Novemba 4, 2021 kuwa Sabaya ni mgonjwa na wamepokea taarifa hizo leo asubuhi.

Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Patricia Kisinda amekubali maombi hayo na kuahirisha kesi hiyo hadi kesho Novemba 4.