Mahakama Kuu Kanda ya Arusha nchini Tanzania, imepokea maombi ya rufaa ya aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili ambapo tarehe 15 Oktoba 2020 walihukumiwa kifungo cha miaka 90 jela.

Mbali na Sabaya, wengine ni Silvester Nyegu (26) na Daniel Bura, kila mmoja amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia kwenye makosa matatu ya ujambazi na unyang’anyi wa kutumia silaha.

Sabaya amekata rufaa hiyo huku akiendelea na kusikiliza kesi yake nyingine inayomkabili ya uhujumu uchumi.

Katika rufaa hiyo ambayo tayari imeshapokelewa, Sabaya amewasilisha sababu zaidi ya kumi za kupinga hukumu hiyo ambayo itamuweka gerezani kwa miaka 30.

Rufaa hiyo ambayo imepokelewa mwishoni mwa wiki na kusajiliwa kwa namba 129/2021, inatokana na kesi ya jinai namba 105/2021 ambayo ilisikilizwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo.

Akizungumza kwa niaba ya mawakili wa waleta rufaa hao, Wakili Moses Mahuna alisema kuwa kwa sasa wanasubiri kupewa wito wa mahakama kwa ajili ya kuanza kwa shauri hilo.