Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita leo Alhamisi Novemba 4, 2021, imeahirishwa tena baada ya mtuhumiwa huyo wa kwanza kudaiwa kuendelea kuumwa.

 Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilipanga shauri hilo namba 27, 2021 kuendelea kusikilizwa leo ambapo shahidi wa saba wa jamhuri ambaye ni Ofisa wa Tehama wa Benki ya CRDB Kanda ya Kaskazini, Jofrey Nnko angeendelea kutoa ushahidi wake.

Akizungumza leo mahakamani hapo, Wakili Mosses Mahuna anayemtetea Sabaya aliieleza mahakama kuwa mtuhumiwa huyo wa kwanza bado ni mgonjwa na kuwa ametoa ruhusa kesi hiyo iendelee kusikilizwa bila yeye kuwepo.
 

Hii ni mara ya pili mtuhumiwa huyo kushindwa kufika mahakamani hapo ambapo jana Novemba 3 pia alishindwa kufika mahakamani akidaiwa kuumwa akiwa gerezani.
 

Wakili wa Jamhuri, Ofmed Mtenga aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi ruhusa ya maandishi ya mtuhumiwa ya shauri kuendelea bila yeye kuwepo iwasilishwe mahakamani hapo.
 

Hakimu Kisinda alikubaliana na maombi hayo na kuahirisha kesi hadi kesho itakapoendelea na usikilizwaji baada ya kibali cha maandishi cha mtuhumiwa huyo kuruhusu kesi hiyo iendelee bila yeye kuwepo kitakapowasilishwa mahakamani hapo.