Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa zaidi ya mara tano imeshindwa kuanza kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya kughushi cheti cha ndoa inayomkabili Khairoon Jandu.

Hatua hiyo imekuja kufuatia wakili wa washtakiwa Abubakar Salim kutofika mahakamani na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuliitisha jalada la kesi hiyo ofisini kwake.

Awali ilidaiwa kuwa upelelezi dhidi ya kesi hiyo ambayo inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Joseph Lwambano ulikwisha kamilika na mashahidi kuandaliwa kwa ajili ya kuanza kutoa ushahidi wao lakini imeahirishwa tena mpaka Novemba 29, mwaka huu ili kuangalia kama DPP atakuwa amerejesha jalada la kesi hiyo mahakamani hapo ama la.

Awali kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa kwa mfululizo kuanzia Novemba Mosi /2 na 3/2021 ambapo mashahidi wa upande wa mashtaka walikwisha andaliwa na wakili wa serikali Ashura Mzava miongoni mwa mashahidi hao yumo Wakili wa kujitegemea Jerome Msemwa lakini ilishindikana baada ya DPP kuliitisha jalada la kesi hiyo.

Msemwa ambaye ni shahidi wa upande wa mashtaka alitarajiwa kuanza kutoa ushahidi wake kwenye kesi hiyo ya kughushi cheti cha ndoa inayomkabili Khairoon Jandu Novemba Mosi mwaka huu lakini alikwama kufuatia hatua hiyo ya kuitishwa kwa jalada.

Awali kabla ya jalada la kesi hiyo kuitishwa na DPP kesi hiyo ilikwama kuanza kusikilizwa kwa sababu wakili mshtakiwa, Abubakar Salim alikuwa na udhuru …Kwa mujibu wa taarifa iliyofikishwa mahakamani hapo wakili huyo alikwenda kuhudhuria kesi Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi.

Kufuatia taarifa hiyo,Wakili wa serikali Ashura Mzava alidai ni mara ya tano sasa kesi inashindwa kuanza kusikilizwa kwa sababu ya wakili wa utetezi kutofika mahakamani.

“Mheshimiwa hakimu pamoja na wakili kuleta taarifa hii lakini naona kuna mchezo anafanya hii ni mara ya tano sasa kesi inashindwa kuendelea kwa yeye kutofika mahakamani naandaa mashahidi lakini wakili haonekani mahakamani” alidai wakili Mzava.

Katika kesi hiyo Khairoon anadaiwa katika tarehe na mwezi usiofahamika mwaka 2020, jijini Dar es Salaam kwa njia ya udanganyifu alighushi cheti cha kuzaliwa cha mtoto Gurditsing Jandu, akionyesha kuwa kimetolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) wakati akijua kuwa ni uongo.

Katika shtaka lingine, Khairoon anadaiwa kuwa katika tarehe na mwezi usiofahamika mwaka 2020 alighushi cheti cha ndoa akionyesha kimetolewa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania Bakwata jambo alilojua kuwa sio kweli.